Sio kweli! Rais Samia hakupongeza uteuzi wa Karua

Muhtasari

•Ujumbe huo ulionyesha kama kwamba rais Samia aliridhishwa sana na uamuzi wa kinara huyo wa ODM.

•Serikali ya Tanzania kupitia kwa msemaji wake Gerson Msigwa pia imejitokeza kutupilia mbali ujumbe huo.

Rais Samia Suluhu na Martha Karua
Rais Samia Suluhu na Martha Karua
Image: HISANI

Ujumbe wa Twitter ambao umekuwa ukisambaa kwenye mitandao ya kijamii ukionyesha kuwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameidhinisha uongozi wa mgombea urais wa muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga na mgombea mwenza wake Martha Karua ni ghushi.

Ujumbe huo ambao ulianza kusambaa punde baada ya Raila kutangaza uteuzi wa Karua kama mgombea mwenza wake ulionyesha kama kwamba rais Samia aliridhishwa sana na uamuzi wa kinara huyo wa ODM.

Pia uliashiria kama kwamba rais Samia aliwasihi Wakenya kuwapigia kura Raila na Kalonzo katika uchaguzi wa Agosti 9.

"Nimepokea kwa furaha habari za uteuzi wa mama @MarthaKarua kama mgombea mwenza wa @RailaOdinga. Mama Karua anatambulika kote Afrika kwa kazi yake nzuri na ataifaa sana taifa la Kenya. Nawaomba wakenya waitumie vyema nafasi ya mabadiliko," Ujumbe huo ghushi ulisoma.

Baada ya uchunguzi wa kina tumeweza kubaini kuwa rais Samia hakuchapisha ujumbe wowote katika ukurasa wake wa Twitter siku ya Jumatatu.

Ujumbe wa mwisho wa Samia kwenye Twitter ulikuwa wa kumpongeza rais mpya wa UAE Mohamed Bin Zayed kwa kuchaguliwa kwao.

Serikali ya Tanzania kupitia kwa msemaji wake Gerson Msigwa pia imejitokeza kutupilia mbali ujumbe huo. Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Msigwa alisema ujumbe huo ghushi ulikuwa na nia mbaya ya kisiasa.

"Wazazi na Jamii tuzungumze na vijana wanaotumika kufanya uhalifu huu WAACHE MARA MOJA. Kwa kuwa wahusika wote hukamatwa na kusababisha usumbufu kwa wazazi na jamii.Waliokamatwa wengi wao ni vijana wanaotumiwa na watu wenye maslahi yao na wanapokabiliana na mkono wa sheria hutelekezwa na waliowatuma" Alisema Msigwa.

Martha Karua mwenyewe alianguka kwenye mtego wa ujumbe huo kwani aliuzungumzia akiwa katika mahojiano na Citizen TV.

"Nimefurahi pia kuona ujumbe wa Twitter wa rais wa Tanzania akitupongeza kwa tikiti hii," Karua alisema.