Wakana Mungu wamtaka Sakaja afunge makanisa yenye kelele

Muungano huo umempa Sakaja muda wa siku saba kuchukua hatua.

Muhtasari

•Wakana Mungu  wamemtaka Sakaja kubatilisha ilani ya kufungwa kwa maeneo ya burudani yenye kelele na kutoa mpya itakayojumuisha makanisa yenye kelele.

•Sakaja alibatilisha leseniza maeneo yote ya burudani yanayoendeshwa ndani ya maeneo ya makazi na kuwaelekeza wafanye kazi katika CBD pekee.

Harrison Mumia
Image: Instagram

Muungano wa Wakana Mungu nchini Kenya wamemtaka Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja kubatilisha ilani ya kufungwa kwa maeneo ya burudani yenye kelele na kutoa mpya itakayojumuisha makanisa yenye kelele.

Muungano huo umempa Sakaja muda wa siku saba kuchukua hatua na kutishia kuenda mahakamani kutafua mwongozo wake juu ya hilo iwapo halitatimizwa.

Katika barua ambayo aliyoandika Ijumaa, Desemba 2, Rais wa Muungano hupo Harrison Mumia alisema uamuzi wagavana unahitajika kutoegemea upande wowote na sio kuwabagua wafanyabiashara.

"Tunaomba ubatilishe ilani yako ya umma ya Novemba 25, na utoe toleo jipya la kujumuisha jumuiya ya kidini ndani ya siku 7, ili ionekane kuwa unashughulikia suala la kelele bila upendeleo," Mumia alisema.

Gavana Sakaja alibatilisha leseniza maeneo yote ya burudani yanayoendeshwa ndani ya maeneo ya makazi na kuwaelekeza wafanye kazi katika CBD pekee.

Hii, alisema, ililenga kuzuia kelele.

Aliagiza zaidi kuwa vilabu vilivyo karibu na makazi ya watu vinapaswa kuacha kucheza muziki ifikapo saa nne usiku.

"Uchezaji wa muziki lazima usitishwe ifikapo saa nne usiku na maduka yote ya pombe yatoe nafasi ya maegesho kwa wateja wao kwa sababu tutazuia magari yanayosababisha vikwazo kando ya barabara na njia za miguu," Sakaja alisema.

Siku ya Alhamisi, alisema kuwa mashirika ya kidini hayatakabiliwa na kufungwa kwa sababu ya uchafuzi wa kelele lakini yatahitajika kutii sheria.

"Sitafunga makanisa. Tunataka yaeneze injili juu ya kutii sheria na kanuni," alisema

"Hata hivyo, nitaanzisha mazungumzo nao kwa sababu lazima tuwe na busara na tukubaliane mjini."

Jumuiya ya Wasioamini Mungu ilisema ilitarajia ofisi ya gavana kuzingatia Kifungu cha 27 (4) cha Katiba.

Kifungu hicho kinasema kwamba "Nchi haitabagua mtu yeyote moja kwa moja au kwa njia yoyote kwa misingi yoyote ikiwa ni pamoja na rangi, jinsia, ujauzito, hali ya ndoa, hali ya afya, kabila au asili ya kijamii, rangi, umri, ulemavu, dini, dhamiri, imani, utamaduni. , mavazi, lugha au kuzaliwa."