Uhuru apongeza vijana kwa ubunifu

Muhtasari

Uhuru alisema hayo baada ya kuzuru maonyesho ya ubunifu uliofanywa na vijana stadi kwa teknolojia.

Rais alikuwa katika Chuo cha Shirika la Wanyama wa Pori huko Manyani, Kaunti ya Taita Taveta

Rais Kenyatta alisema vijana hao wamepunguza gharama za kutambua rasilimali zilizo humu nchini 

Rais Uhuru Kenyatta katika chuo cha KWS cha Manyani. Picha:PSCU
Rais Uhuru Kenyatta katika chuo cha KWS cha Manyani. Picha:PSCU

Rais Uhuru Kenyatta amepongeza vijana kwa kuwa mstari wa mbele katika ubunifu wa kiteknolojia ambao unanuia kuleta mabadiliko kwa kutoa suluhisho kwa matatizo nchini. 

Akizungumza siku ya Ijumaa rais alielezea kuridhika kwake kwamba kupitia ubunifu stadi wa vijana, Kenya imeafikia lengo lake la kufanya uchumi, jamii na serikali kuwa za kidijitali na kubuni mfumo wazi katika utoaji wa huduma bora kwa wakenya.

“Kufikia wakati huu mwaka ujao ambapo uchoraji wa ramani zetu utakapokamilika na kumaliza zoezi la kutambua na kuratibisha rasilimali za Kenya zilizo chini ya ardhi na tutakapondelea kufanikisha mitandao ya kidijitali,  Kenya itabadilika kabisa. "Hakika, , Kenya itakuwa imara katika njia ya kuafikia mabadiliko ya kweli ambayo hayajatolewa nchi za kigeni lakini yaliyobuniwa na kustawishwa na vijana wetu wenyewe. Hili ni jambo linalonipa fahari ya kweli,” kasema Rais.

Uhuru alisema hayo katika Chuo cha Shirika la Wanyama wa Pori huko Manyani, Kaunti ya Taita Taveta, baada ya kuzuru maonyesho ya ubunifu uliofanywa na vijana stadi kwa teknolojia.

Maonyesho hayo chini ya maudhui 'Na Wakenya, Kwa Wakenya’ yaliyohusu miradi ya usoroveya, upigaji picha za usoroveya kwa kutumia vyombo vya angani, mipaka, mitandao na usalama wa kitaifa.

Rais  Kenyatta alisema kinyume na wazo lililo na baadhi ya watu, serikali haitumii mashirika ya kigeni kutekeleza baadhi ya mipango yake muhimu kama vile Huduma Namba na zoezi la mwaka uliopita la kuhesabu watu.

Kuhusu utambuzi kwa kutumia teknolojia, Rais Kenyatta alisema vijana hao, kwa mara ya kwanza katika eneo hili, wamefanya shughuli za kutambua rasilimali zilizo humu nchini kwa kutumia asilimia kumi pekee ya kiasi cha shilingi bilioni 30 ambazo kampuni za kigeni zilikuwa zimeitisha kuifanya kazi hiyo. 

“Kuanzia maji hadi dhahabu na madini ya chuma, tutajua kilicho chini ya ardhi zetu. Hii ndio itakayotupatia nafasi ya kuimarisha rasilimali hizi kwa maslahi bora ya wakenya milioni 50,” Uhuru alikariri.  

Kuhusu ukusanyaji ushuru, Rais Kenyatta alisema kazi ya maeneo mbali mbali ya jiografia iliyopigwa picha za angani inayofanywa na vijana kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1972 itaimarisha ukusanyaji ushuru na kuboresha uwezo wa serikali wa kutoa huduma kikamilifu.