Kizungumkuti cha COVID-19 kwa sekta ya elimu

Muhtasari

• Kenya yakodolea macho hofu ya mlipuko wa pili wa maambukizi ya Covid-19.

• Wasimamizi wa vyuo vikuu nchini wameanza kutafakari kuhusu hali itakavyokuwa ikiwa maambukizi ya virusi vya corona yatazidi.

• Waziri Kagwe alitoa onyo kali kwa wananchi wasiozingatia masharti ya kuthibiti maambukizi ya virusi vya corona.

 

Waziri wa Elimu George Magoha
Waziri wa Elimu George Magoha
 

Wanafunzi wa mwaka wa mwisho katika vyuo vikuu nchini wameingiwa na hofu majuma mawili tu baada ya kurejelea masomo yao huku taifa likikodolea macho hofu ya mlipuko wa pili wa maambukizi ya Covid-19.

Wasimamizi wa vyuo vikuu nchini wameanza kutafakari kuhusu hali itakavyokuwa ikiwa maambukizi ya virusi vya corona yatazidi licha ya kwamba bado wanajizatiti kuwatayarisha wanafunzi wao kukamilisha silabasi ili wafuzu.

“Jamani tupewe muda tukamilishe mtihani wetu tuondoke.Tunazingatia masharti tuliyopewa ya kunawa mikono na kuvalia maski,” Kelvin Muthii, mwanafunzi wa Chuo kikuu cha Maasai Mara alilalama.

 

Hofu hata hivyo imekithiri miongoni mwa wanafunzi na wazimamizi wa taasisi za elimu baada ya wizara ya afya kutishia kufunga taasisi zote za masomo nchini ikiwa idadi ya maambukizi itazidi kuongezeka kasi, sikuchache tu baada ya kuzifungua.

Kwa majuma machache sasa visa vya maambukizi ya virusi vya korona vimekuwa vikiongezeka kwa kasi hali ambayo imezua tumbo joto miongoni mwa wadau wa sekta mbali mbali za kiuchumi na kupelekea wizara ya kafya kutishia kutangaza masharti mapya ya kudhibiti maambukizi.

Waziri wa afya Mutahi kagwe siku ya Jumapili alitoa onyo kali kwa wananchi wasiozingatia masharti ya kuthibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Wanafunzi wa chuo kikuu wakifuzu. Picha; Maktaba
Wanafunzi wa chuo kikuu wakifuzu. Picha; Maktaba

Hata hivyo kile waziri hakutaja ni kwamba wananchi wamekuwa wakiiga mifano ya viongozi wao ambao mara kwa mara wameonekana katika maeneo ya hadhara na katika mikutano ya kisiasa wakikiuka kanuni za kudhitibi maambukizi ya covid-19.

Swali ni Je! Maambukizi yakiendelea kuongezeka shule na taasisi zingine za masomo zitafungwa au la na ikiwa zitafungwa basi zitafungwa kwa muda upi?.

Baadhi ya wataalam wa afya ya umma na wanauchumi wameonya dhidi ya kurejesha masharti makali ya kudhibiti virusi vya corona wakisema kwamba yafaa tukubali kuishi na maradhi hayo kwa sababu hayataisha leo wala kesho.

Hofu ya wazazi wengi hata hivyo ni kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari huku wao wakielezea wasi wasi kwamba huenda watoto wao wakaambukizwa virusi vya corona wakiwa shuleni.

 

Ni wanafunzi wa kidato cha nne, darasa la nane na wale wa darasa la nne walioruhusiwa kurejea shuleni pekee. Serikali ilikuwa bado inapanga mikakati ya kuruhusu wanafunzi wa madarasa mengine kurejea shuleni.

Hapa Kenya wataalam wa afya na washauri wa serikali wameonya kuwa taifa limeanza kushuhudia mkurupuko wa pili wa maambukizi wakitaja kulegezwa kwa masharti ya kudhibiti maambukizi ya virusi hivi kama sababu kuu.

Waziri wa elimu nchini Profesa George Magoha aliagiza kufunguliwa kwa vyuo vikuu nchini mnamo Oktoba 5, 2020 ili kutoa fursa kwa wanafunzi wa mwaka wa mwisho kukamilisha masomo yao baada ya  kuwa nyumbani muda wa miezi sita.

Hatua ya kufunguliwa kwa taasisi za elimu ilichochewa na kupungua kwa idadi ya maambukizi nchini na vile vile kuongezeka kwa idadi ya watu waliokuwa wakipona maradhi haya.

Kulingana na shirika la afya duniani (WHO) hali ya kawaida ya maambukizi inafaa kutangazwa ikiwa maambukizi yatapungua hadi chini ya asilimia tano kwa muda wa majuma kadha.

Kulingana na waziri wa afya Mutahi Kagwe, huenda taifa likalazimika kurejesha masharti makali ya kudhibiti maambukizi ya corona ikiwemo kufunga maeneo ya burudani, masoko, makanisa, kuongeza muda wa kafyu miongoni mwa vikwazo vinginevyo.

Kuhusu usalama wa wanafunzi ambao wamerejelea masomo waziri Kagwe alisema kwamba wizara yake itaanza kuangazia hali ya maambukizi ya Covid-19 katika shule na taasisi zote za masomo nchini ili kudhibiti ueneaji wa virusi hivyo miongoni mwa wanafunzi.

“Tutazidi kumulika hali ilivyo katika shule zetu ili kuwezesha maamuzi yenye busara hapo baadaye,” alisema Kagwe.

Mwandishi Dan Mwenda ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Maasai Mara.

(Mhariri Davis Ojiambo)