Ajisalimisha kwa polisi baada ya kumuua mchumba wake kwa Kisu

Muhtasari

• Mwanamke alimdunga mchumba wake kisu hadi kufa huko Kericho.

• Inasemekana wawili hao wamekuwa na migogoro ya kifamilia kwa muda sasa.

Crime scene
Crime scene

Wakazi wa eneo la Kapsoit katika kaunti ndogo ya Ainamoi wamepatwa na mshangao baada ya mwanamke mmoja kumdunga mumewe kisu hadi kifo.

Walioshuhudia kisa hicho walisema kwamba wapenzi hao wamekuwa na migogoro kwa wiki moja iliyopita.

Wapenzi hao wanasemekana kuishi katika nyumba moja ya kukodi eneo hilo, na mwanamke huyo aliibua vurugu baada ya mpenziwe kumuajiri mwanamke mmoja kusimamia mashine zake za kucheza kamari ambazo zilikuwa zikihudumu katika soko hilo.

Baadaye mwanamke huyo anasemekana kuzua vurugu na kumdunga mwanaume huyo kisu shingoni na kifuani na kumuua papo hapo.

Wenyeji walifika katika eneo la mkasa ili kuokoa maisha ya mfanyibiashara huyo ambaye alikuwa amepata majeraha mwilini mwake.

Pindi tu alipokamilisha kitendo hicho cha unyama, mwanamke huyo, 24 , aliondoka eneo hilo kutumia bodaboda na kujisalimisha katika kituo cha polisi cha Ainamoi.

Maafisa wa polisi walifika eneo la mkasa mara moja na kuupeleka mwili wa marehemu katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya rufaa ya Kericho.

Kulingana na taarifa ya polisi, mwanamke huyo atazuiliwa huku akisubiri kufikishwa mahakamani.