Bangi, ufugaji wa nyoka hautasuluhisha matatizo ya Wakenya-Miguna amwambia Wajackoyah

Muhtasari
  • Alitoa maoni kuwa nchi nyingi zimehalalisha bangi lakini hiyo haijaifanya dawa hiyo kuwa mtaji wao mkuu wa kiuchumi
  • Mwanasheria huyo alisema hata nchi nyingi zinazolima bangi duniani kote hazijaendelea zaidi
Mgombea urais Wajackoyah,wakati wa mahojiano na Radiojambo 10/juni/2022
Image: CHARLENE MALWA

Wakili Miguna Miguna amemrushia vijembe mgombeaji Urais wa Chama cha Roots kwa kushikilia manifesto yake ya kiuchumi kuhusu bangi na ufugaji wa nyoka.

Katika jumbe kwenye ukurasa wake wa twitter siku ya Jumamosi kuhusiana na maoni yake kuhusu suala hilo, wakili huyo alisema matatizo ya Wakenya yanapita zaidi ya ukulima wa bangi na nyoka.

Miguna wakati uo huo alionekana kutokubaliana na msemo wa Wajackoyah wa kusimamisha katiba ya Kenya akisema hilo litakuwa kinyume cha sheria.

"Hautarekebisha Kenya kwa kupindua Katiba ambayo watu walijipa wenyewe mnamo 2010," aliandika.

"Huwezi kutatua mgogoro wa madeni ya jinai kwa kuuza sumu ya nyoka. Kutumia, sababu, mantiki na maono ndiyo suluhu."

Alitoa maoni kuwa nchi nyingi zimehalalisha bangi lakini hiyo haijaifanya dawa hiyo kuwa mtaji wao mkuu wa kiuchumi.

Mwanasheria huyo alisema hata nchi nyingi zinazolima bangi duniani kote hazijaendelea zaidi.

"Bangi imehalalishwa katika nchi nyingi ikiwa ni pamoja na Kanada, baadhi ya majimbo nchini Marekani na baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya. Lakini hiyo haijaifanya bangi kuwa mtaji wa kiuchumi. ," aliongeza.

Aliongeza kuwa ili Wakenya warudi nyuma kiuchumi, ni sharti utawala unaofuata uweke kipaumbele kunyakua ardhi na utajiri wote ulioibwa.

Hii, alisema, itaiwezesha nchi kuwa na uwezo wa kulipa madeni yake kwa urahisi.

"Kampeni kuhusu upumbavu kuhusu bangi, ufugaji wa nyoka na mambo mengine ya kipuuzi ni woga," Miguna alisema.

"Matatizo ya Kenya hayahitaji kufanya kitu chochote kichaa au kijinga. Inahitaji tu kutoogopa, maono na ajenda ya kuleta mabadiliko."