Maaskofu wamshambulia Wajackoyah kuhusu uhalalishaji wa bangi

Muhtasari

•Baraza la Maaskofu wa Kikatoliki nchini Kenya lilisema Wakenya hawafai kuwapigia kura wanasiasa wanaopendekeza sera zinazolenga kuhalalisha matumizi ya dawa za kulevya.

•Muheria pia aliwataka wapiga kura kuwakataa viongozi wanaounga mkono uavyaji mimba na walio na ajenda ya kuhalalisha tabia zilizoharamishwa za ngono zikiwemo ponografia.

Archbishop Antony Muheria
Archbishop Antony Muheria
Image: EUTYCAS MUCHIR

Jumapili maaskofu wa Kikatoliki walivunja ukimya wao kuhusu kampeni za kisiasa zinazoendelea na kuwataka wapiga kura kukataa mapendekezo yasiyo ya kawaida ya wagombea. 

Katika shambulio fiche kwa mgombea urais wa Roots Party George Wajackoyah, Baraza la Maaskofu wa Kikatoliki nchini Kenya lilisema Wakenya hawafai kuwapigia kura wanasiasa wanaopendekeza sera zinazolenga kuhalalisha matumizi ya dawa za kulevya.

Wajackoyah ameahidi kuhalalisha bangi iwapo atashinda kiti cha urais, akitaja kuwa ina manufaa ya kiafya na kiuchumi.

Amesema atageuza ekari za mashamba kuwa mashamba ya bangi na kutumia mapato hayo kulipa deni la Kenya. Kwa sasa matumizi ya bangi yamepigwa marufuku nchini Kenya.

Askofu Mkuu wa Nyeri Anthony Muheria ambaye alizungumza kwa niaba ya makasisi hao pia aliwataka wapiga kura kuwakataa viongozi wanaounga mkono uavyaji mimba na wale walio na ajenda ya kuhalalisha tabia zilizoharamishwa za ngono zikiwemo ponografia.

Alisema viongozi wanaounga mkono ajenda zisizo za kimaadili hawatakuwa na dhamiri na wataleta maangamizi kwa jamii.

Viongozi hao wa kidini pia wanataka wapiga kura kuwakataa viongozi wafisadi. Muheria aliwashauri wapiga kura kutafuta viongozi wanaojitolea kupigana na maovu na wanaotoa hatua madhubuti za jinsi ya kufanya hivyo.

“Tunawaomba mkatae kumchagua kiongozi yeyote ambaye tunaona ataeneza saratani ya ufisadi. Kiongozi anayechaguliwa anapaswa kuchukia rushwa katika ngazi zote na awe mfano kwa wengine,” alisema

Muheria alizungumza katika Kanisa Kuu la Kikatoliki la Consolata huko Nyeri siku ya Jumapili.

Muheria aliongeza kuwa ni lazima kiongozi awe mtu anayeheshimu sheria za Mungu na ambaye ataendeleza maadili ya kitamaduni ya Kiafrika na ya Kikristo.

Muheria aliwaomba Wakenya kumchagua kiongozi wa utumishi mwenye maono, anayepatanisha na muaadilifu wa hali ya juu.

“Ni muhimu tuwahoji wagombeaji wote kuhusu msimamo wao kuhusu masuala ya maadili na maadili. Tunaweza kuangalia kauli zao za awali na kuwauliza waeleze wanachokisimamia.”

Ili taifa liweze kustawi, alisema, ni lazima liwekwe kwa misingi mizuri ya kimaadili.

Alisema inasikitisha kwamba baadhi ya viongozi wanaendelea kupendekeza, katika ajenda zao, kuenezwa kwa sera chafu na zisizo na maadili.

(Utafsiri: Samuel Maina)