'Mungu anawaona,'Seneta Susan Kihika ajibu madai kwamba yeye sio Mkenya

Muhtasari
  • Seneta Susan Kihika ajibu madai kwamba yeye sio Mkenya
Seneta wa Nakuru Susan Kihika
Image: Hisani

Seneta wa Nakuru Susan Kihika amejibu ombi lililowasilishwa la kutaka kuzuiwa kwa ombi lake la ugavana kwa misingi kwamba yeye si raia wa Kenya.

Akitumia ukurasa wake wa twitter Jumanne jioni, Kihika alikejeli madai hayo akidokeza kwamba mzozo huo wa uraia uliletwa tu na watu ambao wanamtaka kuacha matarajio yake.

Anahoji zaidi jinsi madai hayo yanaibuka wakati anatafuta kiti cha Gavana wa Nakuru, lakini hayakutolewa alipowania kiti cha Seneti.

"Soo....Kama Seneta nilikuwa Mkenya lakini sasa ninaenda kugombea Ugavana si Mkenya. Ni sawa; Mungu anawaona," aliandika kwenye Twitter.

Maoni yake yanakuja baada ya Joseph Kimani Njuguna Jumanne kuwasilisha ombi mbele ya Tume Huru ya Uchaguzi (IEBC) akitaka azuiwe kushiriki uchaguzi wa Agosti.

Mlalamishi huyo anadai kuwa Seneta huyo aliuacha uraia wake wa Kenya mwaka wa 2003 kwa ajili ya uraia wa Marekani.