Justina Wamae amezea mate nafasi ya uwaziri katika serikali ijayo

Mgombea mwenza huyo wa Roots Party alidokeza kuwa angependa kupata nafasi katika wizara ya kilimo.

Muhtasari

•Justina alidokeza mpango wake wa kuomba nafasi ya umma katika serikali ijayo baada ya jaribio lake la kuwa naibu rais wa pili wa Kenya kufeli.

•Justina alisema kuwa utumishi wa umma umekuwa shauku yake kwa muda mrefu na kudai anatamani sana kupata nafasi.

akipiga kura katika kituo cha Syokimau Bore hole huko Mavoko, Kaunti ya Machakos Jumanne, Agosti 9, 2022.
Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Roots Justina Wamae akipiga kura katika kituo cha Syokimau Bore hole huko Mavoko, Kaunti ya Machakos Jumanne, Agosti 9, 2022.
Image: GEORGE OWITI

Aliyekuwa mgombea mwenza wa Roots Party Justina Wangui Wamae ameeleza ndoto yake ya kuhudumu katika serikali ya Kenya.

Katika mahojiano na waandishi wa habari siku ya Alhamisi, Justina alidokeza mpango wake wa kuomba nafasi ya umma katika serikali ijayo baada ya jaribio lake la kuwa naibu rais wa pili wa Kenya kufeli.

"2017 nilikuwa nimesimama kuwania kiti cha ubunge cha Mavoko na nikaanguka, 2018 nikaomba nafasi ya Katibu wa Kudumu (PS). Kwa hivyo ile serikali itaingia inahitajika kutangaza nafasi ya PS na CS, nitaomba," Justina alisema.

Mgombea mwenza huyo wa Profesa George Wajackoyah alibainisha kuwa iwapo atakosa kupata nafasi atakubali hatima yake.

Justina alidokeza kuwa angependa kupata nafasi katika wizara ya kilimo.

"Kilimo ni sawa ndio tufanya miradi. Na ndio hata tuweze kufanya jaribio la mradi wa kukuza bangi ya mauzo ili vijana waone kama wataweza kujisimamia," Alisema.

Justina alisema kuwa utumishi wa umma umekuwa shauku yake kwa muda mrefu na kudai anatamani sana kupata nafasi.

Aidha alieleza furaha yake kubwa kuona baadhi ya Wakenya wakipendekeza apatiwe nafasi ya uongozi katika serikali ijayo.

"Nitaomba kazi kama Mkenya mwingine yeyote na nikipatiwa fursa hiyo sitakataa kwa sababu napenda utumishi kwa umma,"

Mapema wiki hii chama cha Roots kilimtimua Justina kama naibu kiongozi na kumteua Vinod Ramji kama Naibu Kiongozi mpya.

Haya yalitokea siku chache tu baada ya kiongozi wake George Wajackoyah na Justina kutofautiana kwa madai kuwa anawakilisha vibaya msimamo wa chama.

Chama hicho kilisema mabadiliko hayo yanafuatia azimio la Halmashauri Kuu ya Taifa katika kikao kilichofanyika katika ofisi kuu ya chama mjini Karen.

“Tunarejea suala lililotajwa hapo juu kufuatia azimio la Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Roots katika kikao kilichofanyika Makao Makuu ya chama, tunathibitisha uteuzi wa viongozi wapya wa chama,” Sehemu ya taarifa ilisoma.