Mwinjilisti alituambia Uhuru kumtema Ruto ulikuwa mpango wa Mungu - Gachagua

Alisema ilikuwa kazi ya Mungu ili Ruto atakaposhinda, mtu yeyote asiseme ni yeye alimfanya rais.

Muhtasari

• "Tutafanya kazi pamoja na wale waliokuwa washindani wetu ili kulijenga hili taifa pamoja,” Gachagua alisema.

 

Naibu rais mteule Rigathi Gachagua
Naibu rais mteule Rigathi Gachagua

Naibu rais mpya kabisa nchini Kenya, Rigathi Gachagua amedokeza kwamba serikali ya Kenya Kwanza haitokuwa na ubaguzi wowote kwani watafanya kazi kwa pamoja na wale wote waliokuwa wapinzani wao.

Akizungumza katika makazi rasmi ya naibu rais Karen jijini Nairobi wakati wa mkutano wa kutoa shukrani kwa Taifa ulioandaliwa na mrengo huo, saa chache tu baada ya jopo la majaji saba wa mahakama ya upeo kudumisha ushindi wake, Gachagua alisema kwamba hawatakuwa na kinyongo na mtu yeyote.

“Hatuka kitu chochote dhidi ya mtu yeyote. Tutafanya kazi pamoja na wale waliokuwa washindani wetu ili kulijenga hili taifa pamoja,” Gachagua alisema.

Pia alisisitiza kwamba ushindi wa mrengo wa Kenya Kwanza uliwezeshwa na mkono wa Mungu.

Naibu rais huyo alisema kwamba wakati mmoja walihudhuria ibada ya kanisa katika eneo la Kenol ambaye mchungaji mmoja aliwaambia kwamba uamuzi wa rai anayeondoka Uhuru Kenyatta kumtenga naibu wake William Ruto na badala yake kuungana mkono na Raila Odinga ulikuwa ni mpango wa Mungu.

“Ushindi huu ulikuwa ni kazi ya Mungu. Mwinjilisti wa Nigeria alituambia Uhuru alimwacha Ruto kwa sababu yote hayo ni kazi ya Mungu, ili atakapokuwa Rais, hakuna mtu anayeweza kusema alimfanya kuwa rais,” Gachagua alifunguka.

Gachagua alimsifia Ruto kwa kumtaja kuwa mtoto wa mtu asiyekuwa na kitu chochote hatimaye amekuwa rais.

"Kinyume na mipango yote ya watu, kinyume na matumizi ya silaha kubwa zilizowekwa dhidi yetu. leo mtoto wa mtu wa kawaida ambaye babake na mamake hawajulikani hatimaye amekuwa rais," Gachagua alisema.

Gachagua anakuwa naibu wa rais wa pili nchini Kenya chini ya katiba mpya ya mwaka 2010.