"Ombeeni rais Kenyatta," William Ruto awasihi Wakenya

Ruto alisema Kenyatta anahitaji maombi kwa sababu yeye ndiye atasimamia mchakato mzima wa kukabidhi madaraka

Muhtasari

• Ikumbukwe raia Kenyatta amekuwa akisikika kwa mara kadhaa akitoa kauli kwamba hawezi kabidhi madaraka kwa mwizi.

Rais anayeondoka Uhuru Kenyatta na rais mteule William Ruto
Rais anayeondoka Uhuru Kenyatta na rais mteule William Ruto

Rais mteule William Ruto amewataka Wakenya kumuombea kwa sana rais anayeondoka Uhuru Kenyatta ili Mungu ampe busara ya kufanya kukabidhi madaraka kwa njia iliyonyooka isiyo na tashwishi.

Ruto alikuwa akizungumza katika eneo la Njoro kaunti ya Nakuru Jumapili katika ibada ya kutoa shukrani kwa Mungu kwa viongozi wote waliochaguliwa kaunti hiyo kupitia vyama tanzu vya Kenya Kwanza, na haswa chama chake cha UDA ambacho kilinyakua nyadhifa nyingi kaunti hiyo.

“Nataka kuwaomba Muombee raia Uhuru Kenyatta kwa Mungu ili tuwe na kukabidhi madaraka kwa njia ya amani na iliyonyooka kwa sababu yeye ndiye atashiriki mchakato mzima wa kukabidhi,” Ruto alisema.

Ikumbukwe rais Uhuru Kenyatta tangu walipotofautiana na naibu wake mwaka wa 2018, alionekana kumpigia debe Raila Odinga wazi wazi huku akisisitiza kauli ya kwamba hawezi kukabidhi madaraka kwa mwizi.

Wengi wamekuwa wakimhusisha Ruto na kauli hiyo ya wizi, wakisema kwamba bila shaka yoyote kauli hiyo ilikuwa ikimlenga.

Rais Kenyatta alijitoa kimasomaso kumsuta Ruto kwa kampeni zake huku akisema kwamba naibu huyo wake alikuwa anawahadaa wananchi kwa miradi hewa na hata kumtaja kwa majina kama hayo ya mwizi na mwongo.

Watu sasa wanasubiria uamuzi wa mahakama ya upeo adhuhuri hii katika kesi ambayo iliwasilishwa na muungano wa Azumio la Umoja One Kenya kutaka kubatilishwa kwa matokeo ya IEBC yaliyompa Ruto ushindi.

Wengi wanatathmini hali jinsi itakavyokuwa ikiwa mahakama hiyo itadumisha ushindi wa Ruto na wanakisia Rais Kenyatta atakuwa na wakati mgumu wa kukabidhi madaraka kwake haswa kutokana na kauli zake alizokuwa akizitembeza dhidi ya Ruto hapo awali kipindi cha kampeni.