"Mwenye aliphotoshop picha ya marehemu babangu na kuweka sura ya Raila Mungu amsamehe"

Hayo yalikuwa maneno ya huzuni kutoka kwa mchungaji Muthee Kiengei baada ya picha ya babake kutumiwa kumkejeli Raila.

Muhtasari

• “Kampeni zimeisha, maumivu yaliyojitokeza kupitia Photoshop hii hayatawahi kutokea kwa mtu yeyote anayesoma hii" - Muthee Kiengei.

Muthee Kiengei, mtangazaji anayejiongeza kama mhubiri
Muthee Kiengei, mtangazaji anayejiongeza kama mhubiri

Muigizaji ambaye aligeuka kuwa mchungaji Muthee Kiengei amechukizwa na kitendo cha baadhi ya watu kutumia picha ya marehemu baba yake na kuibananga kwa kuifanyia Photoshop ili kuonekana kama ya kinara wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga akipigiwa kwaheri ya kuenda nyumbani baada ya mahakama ya upeo kutupilia mbali ombi lake la kutaka kubatilishwa kwa ushindi wa Ruto.

Kiengei kupitia ukurasa wake wa Facebook, Mtangazaji huyo alionesha kuchukizwa kwake na yule aliyefanya uhariri katika picha ya marehemu babake na kuiwekea sura ya Raila akitembea kwa mkongojo kuashiria kustaafu baada ya kupoteza uchaguzi.

Kiengei hata baada ya kuchukizwa, alisema amechagua kuwasamehe wote waliotumia picha ya babake kueneza dhana ya kisiasa na hivyo kumkosea heshima marehemu mzee wake.

“Kampeni zimeisha, maumivu yaliyojitokeza kupitia Photoshop hii hayatawahi kutokea kwa mtu yeyote anayesoma hii. Kutoka mahali ninapokaa nilichagua kusamehe na kusahau. Tafadhali msamehe kila aliyekuumiza katika msimu wa kampeni na hongera aliyeshinda na aliyeshindwa wakati akijaribu,” Muthee Kiengei aliandika.

Vile vile, mchungaji huyo alimtaka babake kuendelea kupumzika kwa amani na kutomhukumu mtu yeyote aliyefanya kitendo hicho cha kuibua hisia za simanzi na majonzi kwa wapendwa wa marehemu mzee.

“Marehemu Baba yangu....usimhukumu mtu kwa ukali, aliyeihariri baba alikuwa anafanya kazi ya kuweka chakula mezani kwao....walitumia kucheka na kuweka hela zao......Endelea Kupumzika vizuri. Baba,” Kiengei aliandika kwa machungu.