Tukimaliza kuomboleza tutajiunga nanyi kujenga taifa - Donald Kipkorir kwa Kenya Kwanza

“Ndugu William Samoei Ruto, hongera kwa kuwa Rais wetu wa 5" - Kipkorir

Muhtasari

• Lakini Historia haitakuwa nzuri kwa wale wanaomzunguka Baba kila wakati wa Uchaguzi Mkuu - Kipkorir.

Wakili Donald Kipkorir akiwa na rais William Ruto
Wakili Donald Kipkorir akiwa na rais William Ruto
Image: Facebook

Wakili Donald Kipkorir amewataka viongozi na wafuasi wa Kenya Kwanza kuwa wema na wakarimu kwa wafuasi wa Azimio la Umoja One Kenya kufuatia uamuzi wa Mahakama ya upeo uliodunisha ushindi wa William Ruto.

Katika ujumbe ambao aliuandika kwenye ukurasa wake wa Twitter, Kipkorir ambaye ni mkereketwa sugu wa sera za Raila Odinga aliwataka wafuasi wa UDA kutowakejeli wenzao waliopoteza kutoka Kenya Kwanza.

Amesema wanahitaji muda zaidi wa kupona majeraha na maumivu ya kupoteza uchaguzi pamoja na kesi katika mahakama ya upeo kabla ya kujiunga nao katika ujenzi wa taifa.

“Wapendwa kutoka UDA almaarufu Kenya Kwanza, kwa sisi ambao ni mayatima wa Raila ODINGA, mkwasi na shujaa wa taifa anayeishi katika historia ya Kenya, tafadhali kuweni na moyo mkunjufu katika ushindi na mturuhusu kuhuzunika. Baada ya majonzi yetu, tutaungana nanyi katika ujenzi wa taifa. Tulikimbia mbio: tulifanya kila tuwezalo,” Kipkorir aliwaomba mrengo wa serikali.

Jana baada ya mahakama ya upeo kudumisha ushindi wa Ruto, Kipkorir alifichua kwamba amekuwa akimuunga mkono Raila Odinga tangu mwaka 2005 na kusema kwamba kama mkenya halisi mwenye uzalendo wa dhati, ataanza kuinga mkono serikali ya Ruto hata kama hakuwa anampenda kiongozi huyo wa UDA.

“Ndugu William Samoei Ruto, hongera kwa kuwa Rais wetu wa 5. Kama raia halali, ninaahidi utii na uaminifu wangu kwa Urais wako. Mpendwa Raila Amolo Odinga, tangu 2005, nilikupa uungaji mkono wangu wote na wa dhati. Wewe ni Rais wa Kenya utakayekumbukwa milele,” Kipkorir alisema.

Awali kulikuwepo na kurushiana lawana baina ya watu ndani ya Azimio huku baadhi wakilaumiana kutokana na kushindwa kwa kinara wao Raila Odinga.

Kipkorir akizungumzia hili, alisema kwamba baadae muungano huo utafanya marejeleo na kuwatumbua wote waliokuwa wameparamia ili kujinufaisha binafsi.

“Historia itakuwa nzuri kwa Raila Odinga. Ni Rais ambaye hatujawahi kuwa naye. Hatutamsahau Baba. Lakini Historia haitakuwa nzuri kwa wale wanaomzunguka Baba kila wakati wa Uchaguzi Mkuu ili kushinda chaguzi zao wenyewe au kwa faida ya pesa bila kuongeza thamani yoyote kwenye Kura ya Urais,” Kipkorir alizungumza kwa ghadhabu.