Raila ni Kiongozi wangu, lakini nitamkabidhi Ruto madaraka nikitabasamu – Uhuru

Uhuru alikuwa akikutana na viongozi waliochaguliwa na Azimio katika mgahawa wa Maasai Lodge, Rongai

Muhtasari

• Rais Kenyatta alitumia fursa hiyo kumpigia debe Kalonzo kuwa ataendeleza ajenda zao vizuri kama spika wa seneti.

• Farah Maalim alipendekezwa kuwania wadhifa wa naibu spika wa bunge la kitaifa

Rais anayeondoka Kenyatta amesema kiongozi wake ni Raila
Rais anayeondoka Kenyatta amesema kiongozi wake ni Raila
Image: State House Kenya

Rais Uhuru Kenyatta amesema kuwa kiongozi wake atasalia kinara wa Azimio -One Kenya  Raila Odinga, ingawa aliahidi kumkabidhi mamlaka rais mteule William Ruto. 

Ruto alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa Agosti 9 na tume  Huru ya uchaguzi na mipaka nchini (IEBC) na ushindi wake kuidhinishwa na mahakama ya Upeo.

Akizungumza katika mkutano wa wabunge na maseneta waliochaguliwa chini ya mwavuli wa Azimio one Kenya, Uhuru ambaye ndiye mwenyekiti wa Azimio, alisema wamepoteza nafasi ya kuliunganisha taifa kupitia uongozi wa Raila.

“Mlijinyima wenyewe nafasi ya kuliunganisha taifa. Hamjammaliza Raila,” Kenyatta alisema.

Kenyatta aliongeza kuwa kiongozi wake atabaki Baba Raila ila akasema kwamba atamkabidhi Ruto madaraka akitabasamu.

"Nitamkabidhi madaraka nikitabasamu kwa sababu ni jukumu langu Kikatiba kufanya hivyo, lakini kiongozi wangu ni Baba Raila Odinga," rais Kenyatta alisema.

Muungano wa Azimio ambao ulifanyika siku ya Jumatano uliongozwa na viongozi wake mwenyekiti Uhuru Kenyatta, kinara wake Raila Odinga uliandaliwa katika Hoteli ya Maasai Lodge kaunti ya Kajiado.

Viongozi hao walikuwa wakikutana na viongozi wote waliochaguliwa chini ya vyama tanzu vya Azimio One Kenya huku wakitarajiwa kuapishwa kesho Alhamisi katika mabunge yote na pia mchakato wa kuchaguliwa kwa maspika na manaibu wao kufanyika.

Muungano huo ulikubaliana kwa kauli moja kumuunga mkono kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kuania nafasi ya spika wa seneti.  Kalonzo atamenyana na aliyekuwa Gavana wa Kilifi Amason Kingi ambaye ni chaguo la muungano wa Kenya Kwanza Alliance, na Isaac Mwaura.

Muungano wa Azimio pia uliwasilisha jina la Seneta wa Kilifi Stewart Madzayo kwa wadhifa wa Naibu Spika wa Seneti.

Aliyekuwa spika wa bunge la kitaifa , Kenneth Marende atakuwa akipeperusha bendrera ya Azimio kwa wadhifa wa spika wa bunge la kitaifa.

Farah Maalim alipendekezwa kuwania wadhifa wa naibu spika wa bunge la kitaifa chini wa Azimio One Kenya.