Rais Kenyatta, onyesha hadhi katika kushindwa, mpongeze Ruto sasa! - Kabando

“Rais Uhuru, Mheshimiwa: unastahili utulivu, heshima wakati wa kustaafu" - Kabando wa Kabando.

Muhtasari

• "Kenya imekupendelea, imekupa upendeleo kwa njia ya pekee zaidi. Onyesha heshima, unyenyekevu, hadhi katika kushindwa,” Kabando

Raia anayeondoka Kenyatta, aliyekuwa mbunge wa Mukurwweini Kabando wa Kabando na rais mteule William Ruto
Raia anayeondoka Kenyatta, aliyekuwa mbunge wa Mukurwweini Kabando wa Kabando na rais mteule William Ruto
Image: Twitter, State House Kenya

Aliyekuwa mbunge wa Mukurweini kwa muda mrefu Kabando wa Kabando amefunguka mengi kwenye ukurasa wake wa Twitter jinsi walivyomshauri rais anayeondoka Uhuru Kenyatta kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Kabando ambaye ni mmoja wa wandani wa rais Kenyatta na Raila Odinga alisema kwamba kabla ya kampeni, walimshauri rais Kenyatta kutojihusisha na siasa za 2022 kwani angejipaka tope ila rais hakuwasikiliza.

Rais Kenyatta baadae alionekana akimpigia kampeni Raila Odinga wazi wazi licha ya pingamizi kali kutoka kwa Wakenya wengi na hata watu wa eneo lake la Mt Kenya.

Mwanasiasa Kabando aliendelea kueleza kwamba rais Kenyatta hajafanya busara kutompongeza Ruto kwa ushindi kwani hata kama ni aibu, alijitakia mwenyewe.

Alitolea mfano kwamba licha ya kuwa mshindani wake katika uchaguzi wa 2013, Raila Odinga alimtumia risala za pongezi baada ya mahakama ya upeo kutoa uamuzi wa kuithinisha ushindi wake na ni vyema pia yeye kufanya hivo kwa bwana Ruto ambaye ndiye rais mteule anayesubiri kuapishwa Jumanne wiki kesho.

Kwa maana hiyo, Kabando amemtaka rais anayeondoka kwa shruti yoyote ile kunywea na kumhongera Ruto kwani hakuna litakalobadilika, ndiye rais wa Kenya apende akatae.

“Rais Uhuru, Mheshimiwa: Raila alikupongeza kwa uamuzi wa 2013 wa SCoK. Raila alijiunga nawe 2018. Bila shaka, UHURUTO ilikufanya kuwa Rais 2013. Ulikataa ushauri wetu wa kutoshiriki 2022. Uungwana, shukrani, adabu, UTAWALA unadai kwamba sasa umpongeza Rais WSR. Fanya hivo sasa!” Kabando wa Kabando alimtaka Kenyatta.

Alimshauri rais Kenyatta kwamba anastahili amani ya nafsi pindi atakapostaafu na kufanikisha hilo hana budi ila kumhongera Ruto na kurahisisha ugumu uliopo baina yao.

“Rais Uhuru, Mheshimiwa: unastahili utulivu, heshima wakati wa kustaafu. Umefanya sehemu yako, sasa ni wakati wa kuendelea. Usiisugue tena. Usiwape wanaokuchukia sababu ya kukudhalilisha. Kenya imekupendelea, imekupa upendeleo kwa njia ya pekee zaidi. Onyesha heshima, unyenyekevu, hadhi katika kushindwa,” Kabando alitoa ushauri.