Jamaa aliyepakia klipu akisherehekea kushindwa kwa Raila aomba radhi

Niliifanya kama binafsi na sikufanya kwa lengo la kuonesha mrengo wa kampuni kisiasa.

Muhtasari

• Nataka kuomba radhi kwa wateja wetu haswa wale wa Azimio, sikulenga kuumiza hisia za mtu yeyote - Onchiri.

Cliff Onchiri, mfanyikazi wa kampuni ya usafiri wa mabasi ya Transline aliyeonekana kwenye video akisherehekea uamuzi wa mahakama ya upeo kutupilia mbali ombi la Raila Odinga la kutaka kubatilishwa kwa ushindi wa Ruto hatimaye amezungumza.

Baada ya klipu hiyo kusambazwa pakubwa tangu Jumatatu pindi tu baada ya uamuzi, kampuni ya Transline iliachia barua kwa umma ya kuomba radhi kwa wateja wake na kujitenga na klipu hiyo huku ikiahidi kuchukua taratibu za kinidhamu dhidi ya Onchiri.

Onchiri sasa amefunguka kwamba kampuni hiyo ilimfuta kazi na sasa amerudi hatua ya sifuri katika maisha yake.

Katika klipu nyingine ambayo amefanya kwenye TikTok, Onchiri amesikitishwa na kitendo cha ujinga alichokifanya huku akiwa amevaia sare rasmi ya kazi na kuwataka radhi wafuasi wote wa Azimio walichukizwa na kitendo hicho.

“Nataka kuomba radhi kwa video yenye nilifanya kutokana na ujinga wangu. Niliifanya nikiwa katika sare ya kazi. Niliifanya kama binafsi na sikufanya kwa lengo la kuonesha mrengo wa kampuni kisiasa. Nataka kuomba radhi kwa wateja wetu haswa wale wa Azimio, sikulenga kuumiza hisia za mtu yeyote, naomba msamaha sana kwa kile kilichotokea,” Onchiri anaonekana akizungumza kwa huruma kwenye klipu hiyo.

Jana kampuni ya Transline ilitoa taarifa kwa umma ikijitenga na klipu hiyo na sasa inasemekana kwamba jamaa huyo amerudi sokoni kutafuta kazi yoyote ya kumsaidia kukimu mahitaji yake baada ya kudaiwa kuachishwa kazi kutokana na video ile iliyotafsiriwa kama kuiharibia kampuni jina na kuifitinisha na wateja wake ambao ni wafuasi wa mrengo wa Azio.