Koome, Ruto wasema uchaguzi na uamuzi wa kesi ni kutokana na nguvu za Mungu

Koome alikuwa akizungumza katika msiba wa shangazi yake Meru

Muhtasari

• Jumatatu, Koome alitupilia mbali maombi yote yaliyowasilishwa katika mahakama hiyo kupinga ushindi wa Ruto.

Jaji mkuu Martha Koome amekubaliana na Ruto kwamba uchaguzi na uamuzi viliwezesha na Mungu
Jaji mkuu Martha Koome amekubaliana na Ruto kwamba uchaguzi na uamuzi viliwezesha na Mungu
Image: Facebook,Maktaba

Jaji mkuu Martha Koome na rais Mteule William Ruto wote wameonekana kukubaliana katika kitu kimoja kuhusu mchakato mzima wa uchaguzi mkuu wa Agosti 9 – Mungu!

Ruto tangu kutangazwa mshindi mnamo Agosti 15 na mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC amekuwa akinukuliwa kwamba uchaguzi huo pamoja na ushindi wake si kwa njia ya mkato bali ni kwa nguvu ya Mungu aliyeridhia kuwa yeye ndiye atakuwa rais wa 5 wa Kenya.

Ushindi wake ulipingwa mahakamani na makundi ya watu mbali mbali ukiwemo ule muungano wa Azimio ambao walitaka kubatilishwa kwa ushindi wake katika mahakama ya upeo.

Kesi hiyo pia ilitupiliwa mbali na jopo la majaji saba katika uamuzi uliosomwa na jaji mkuu Martha Koome Jumatatu wiki hii na hivyo kuidhinisha ushindi wa Ruto.

Jaji huyo sasa naye amesema kwamba uamuzi walioufanya kutokana na kesi hiyo haukuwa wao bali ni kibali cha Mungu pamoja na busara itokayo Mbinguni.

Koome alikuwa akizungumza kwa mara ya kwanza tangu uamuzi wa mahakama kuu. Alikuwa amehudhuria hafla ya msiba wa shangazi wake huko Meru ambapo alipata nafasi ya kuzungumza.

“Huu (hukumu) ulikuwa ni kwa ajili ya uhuru wa taasisi, hasa Mahakama. Haikutokana na nguvu au uwezo wetu kama mahakama bali ni kwa sababu ya Mungu mwaminifu tunayemtumikia,” Koome alisema.

Jumatatu, Koome alitupilia mbali maombi yote yaliyowasilishwa katika mahakama hiyo kupinga ushindi wa Ruto. Akisoma uamuzi wa jopo la majaji, Koome alisema hakuna hata ombi moja lililokuwa na Ushahidi wa kutosha wa kubatilisha ushindi wa Ruto.

Kufuatia uamuzi huo, Ruto anatarajiwa kuapishwa kama rais wa tano wa Kenya Septemba 13 katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi.