(+video) Sikujua nitarudi kuambia watu zoea sauti ya Ruto - Atwoli ajuta

William Ruto alikuwa na ujuzi wa kisiasa na ujanja wa kufaidi - Atwoli

Muhtasari

• Sisi tulienda kulala tukijua tumeshinda, kumbe sisi tunafanya siasa ambayo haina ujuzi. - Atwoli.

Katibu mkuu wa muungano wa wafanyakazi COTU Francis Atwoli kwa mara ya kwanza kabisa amekubali kwamba ushindi wa Ruto ulikuwa ni mpango wa Mungu.

Atwoli ambaye amekuwa akikashfiwa vikali na kukejeliwa baada ya Ruto kushindwa, haswa kutokana na misimamo yake mikali kwamba Ruto hangeweza kuwa rais wa Kenya, alionekana amenywea na kukubaliana na ukweli huo japo ni mchungu.

Itakumbukwa kauli za Atwoli akimsema vibaya Ruto wakati wa kampeni zilikuwa zinagonga vichwa vya habari kutokana na jinsi alivyokuwa akiweka msisitizo.

Wakati mmoja alinukuliwa akiwaambia watu wa karibu na nyumbani kwa Ruto, Sugoi kukata miti kwani Ruti angejinyonga baada ya matokeo kutangazwa na kupata ameshindwa.

Vile vile moja ya kauli yake ambayo inatumiwa kama utani mpaka sasa ni pale aliwaambia Wakenya kuanza kuzoea sauti ya Raila Odinga mapema kwani kulingana na yeye, Odinga ndiye angekuwa rais na Wakenya wangemsikia kweney runinga na redio kila asubuhi na jioni.

Baada ya Ruto kushinda Odinga, Atwoli ameonekana kubadili msimamo na sasa anasema kwamba kauli zile hazikuwa kutokana na chuki na Ruto bali ilikuwa tu ni moja ya mbinu za kampeni kwa faida ya Raila.

Katika video moja, Atwoli amekubali kwamba Ruto aliwachachafya vibaya sana katika ulingo wa siasa kwani wao kama Azimio walienda kulala wakijua kwamba Odinga ndiye angekuwa rais wao ila wakapatwa na butwaa la karne kutangaziwa Ruto kuwa mshindi na hata mahakama kuidhinisha ushindi wake.

“Mimi niliwaambia mzoee sauti ya Raila Odinga, sikujua nitarudi hapa tena kuwaambia tena mzoee sauti ya Ruto. Mnaona mambo ya Mungu, mnapanga yenu na Mungu anapanga yake. Sisi tulienda kulala tukijua tumeshinda, kumbe sisi tunafanya siasa ambayo haina ujuzi. Na William Ruto alikuwa na ujuzi wa kisiasa na ujanja wa kufaidi,” Atwoli alisema.

Kwa kile kilionekana kama anakubali, Atwoli alisema ni lazima watu wote wamkubali Ruto kama baba wa taifa ili nchi ya Kenya isonge mbele kwa amani.

“Sisi tunakubali kwa sababu hayo yalikuwa matakwa ya Mungu,” Atwoli alisema.