(+video) Siamini tulishindwa, Martha Karua alia, atafakari kuenda mahakama ya haki EA

Karua alisema kwamba hesabu za kura hasa Nairobi haziingiani kwani MCAs wengi ni wa Azimio na kura nyingi za urais zilikuwa zao.

Muhtasari

• Alisema kikubwa kitakachomsukuma kuelekea mahakama ya haki ya EA ni matamshi ya jaji kuhusu uvumi wa hewa moto.

Aliyekuwa mgombea mwenza katika muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Martha karua baada ya kimya tangu mahakama ya upeo kutupilia mbali ombi lao la kutaka kubatilishwa kwa ushindi wa Ruto, sasa amevunja ukimya.

Katika moja ya video inayosambazwa mitandaoni, Karua anaonekana akipinga vikali ushindi wa Ruto pamoja na uamuzi wa mahakama ya upeo akisema kwamba yeye hado hawezi amini Azimio ilishindwa na Kenya Kwanza.

Anasema huenda akatafakari kuelekea katika mahakama ya haki ya ukanda wa Afrika Mashariki ili kutafuta haki baada ya kudai kwamba mahakama ya upeo nchini iliwanyima haki.

“Na Nairobi ambayo inatajwa ni yao, gavana ni wao lakini MCAs wengi ni wa Azimio, kura nyingi za Nairobi za urais zilikuwa ni Azimio. Hizo hesabu haziingiani. Kwa hivyo siwezi nikaamini tulishindwa,” Karua alisema.

Alisema lakini kwa sababu mahakama ilishatoa amri basi hakuna lingine bali ni Kenya kuendelea vile korti iliamuru ila akasema kwamba kuvunjika kwa mwiko si mwisho wa upishi na kudokeza kwamba huenda wakatafakari njia mbadala za kupinga ushindi wa Ruto.

“Kuvunjika kwa mwiko si mwisho wa upishi. Hakuna mahali kwingine tunaweza enda kupinga ushindi wa rais, lakini tunaweza pekeka kule nilikoenda wakati ule mwingine mambo ya haki. Ule uamuzi wa jaji kusema tulikuwa na uvumi wa hewa moto ndio unaweza nipeleka mahakama ya Afrika Mashariki,” Karua aliongeza.

Alisisitiza kwamab binafsi anawaza kuenda katika mahakama ya EA ili kuzungumzia tu ule uamuzi wa uvumi wa hewa moto. Alisema hata hivyo atachukua muda kidogo kutoka siasa ili kupumzika wakisubiri siku 21 zilizoahidiwa na mahakama ya upeo kutoa maelezo zaidi jinsi majaji saba walivyoafikiana na uamuzi wa kumuidhinisha Ruto.

Ikiwa Karua ataenda kwenye mahakama ya haki ya Afrika Mashariki, basi itakuwa ni mara ya pili anafanya hivyo kwani baada ya uchaguzi wa 2017 baada ya mahakama ya juu kutupilia mbali ombi lake la kutaka kubatilishwa kwa ushindi wa gavana wa Kirinyaga Ann Waiguru, amabpo alikuwa mshindani wake, Karua alielekea kwenye mahakama hiyo kutafuta haki.