Rais Kenyatta atakumbukwa kwa kumaliza vita vya baada ya uchaguzi kupitia Handshake - Elachi

Elachi alisema Uhuru alitumia ujanja mkubwa ili kuhaakikisha suluhu la kudumu linapatikana kuhusu vita ya baada ya uchaguzi mkuu.

Muhtasari

• “Rais Kenyatta ameingia katika vitabu vya historia kama mtu mmoja ambaye ameacha Kenya na amefutilia mbali kitu kilikuwa kinaitwa vita vya baada ya uchaguzi,” Elachi alisema.

Beatrice Elachi anasema rais Uhuru Kenyatta atakumbukwa kwa amani baada ya Handshake
Beatrice Elachi anasema rais Uhuru Kenyatta atakumbukwa kwa amani baada ya Handshake
Image: Facebook//Elachi Beatrice

Jumatatu ikiwa siku ya mwisho kwa rais Uhuru Kenyatta kuhudumu katika ikulu kama rais, Wakenya kutoka matabaka mbali mbali wameungana kuzungumzia matukio mbali mbali ambayo rais Kenyatta atakumbukwa nayo katika kipindi cha miaka 10 aliyohudumu kama rais.

Mbunge wa Dagoretti North Beatrice Elachi ni mmoja wa Wakenya hao ambao wamemkumbuka rais Kenyatta kwa mengi.

Akizungumza asubuhi ya Jumatatu katika runinga moja nchini, Elachi alisema kwamba Kenyatta atakumbukwa milele kwa kuleta amani ya kudumu baada ya uchaguzi, kitu amabcho hakijawahi kutokea kila baada ya chaguzi za awali ambapo taifa lingetumbukia katika mzozo.

Elachi alisema kwamba Handshake ya mwaka 2018 kati ya rais Kenyatta na aliyekuwa Waziri mkuu Raila Odinga ndicho kitu ambacho kilisababisha utulivu baada ya uchaguzi mkuu kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa Kenya chini ya katiba mpya.

“Rais Kenyatta ameingia katika vitabu vya historia kama mtu mmoja ambaye ameacha Kenya na amefutilia mbali kitu kilikuwa kinaitwa vita vya baada ya uchaguzi,” Elachi alisema.

Alisisitiza kwamba umpende ama umkatae, rais Kenyatta alikuwa mjanja wa kuhakikisha pande zote zinaridhika.

“Ile Handshake imetuchukua pahali ambapo uchaguzi ambao hakuna risasi la mtutu wa bunduki ya polisi limeenda kwa mtu yeyote,” Elachi alisema.

Mbunge huyo aliyechaguliwa kupitia tikiti ya chama cha ODM alitoa wito kwa uongozi ujao kutovuruga amani ambayo rais Kenyatta alihakikisha imepatikana kutokana na kushikamana kwake na Odinga.