Pauline Njoroge amzomea Babu Owino kwa kusema rais Kenyatta alimcheza Odinga

Hili jambo la kumshutumu Uhuru Kenyatta kwa ujanja linazidi kuudhi - Njoroge.

Muhtasari

• Mtu huyu (Uhuru)  alijitolea kwa uwezo wake wote kwenye kampeni ya Azimio - Njoroge

Njoroge ampasha Owino kwa kumsema rais kenyatta
Njoroge ampasha Owino kwa kumsema rais kenyatta
Image: Facebok

Jana baada ya rais Uhuru Kenyatta kukutana hatimaye na rais anayekuja William Ruto katika ikulu ya Nairobi, mbunge Babu Owino alishindwa kunyamaza baada ya kuona picha za wawili hao waliodhaniwa kuwa mahasimu kusalimiana kwa tabasamu kubwa.

Kwenye mitandao yake ya kijamii, Owino alioneshwa kutofurahishwa kwake na ishara ya Kenyatta kumsalimia Ruto akiwa anatabasamu na kusema kwamba huenda ilikuwa ni njama yake kumchezea shere Raila Odinga ambaye aliangushwa na Ruto.

Owino alisema Kenyatta alicheza njama hiyo na Ruto ili kufeki kama wanahasimiana ili kumcheza Raila.

“Asante Uhuru Kenyatta kwa kuweka neno lako kwa Ruto. Lugha yako ya mwili inaeleza yote. Ilikuw ani uongo mrefu. Bado tutafika tunakokwenda. Kama hatukuweza kuwinda na mbwa tutatumia paka,” Owino aliandika.

Matamshi haya ya Owino hayakupokelewa na baadhi ya wanablogu wanaoegemea upande wa Ruto ambapo walionesha kutoridhishwa kwake na kile walisema Owino anamshambulia rais Kenyatta.

Mwanablogu Pauline Njoroge alimtetea vikali rais Kenyatta kwa kusema kwamba hakumcheza Odinga hata kidogo bali ni watu haswa kutoka ngome yake ya Nyanza ambao walilala na hawakujitokeza kwa wingi kumpigia kura.

Alizidi mbele kumzomea Owino kwamba iwapo watu wa ngome ya Odinga wangejitokeza basi hadithi ya kura laki mbili ambazo Ruto alimshindia Odinga nazo haingekuwa inazungumziwa kwani Odinga angeibuka mshindi mapema.

“Hili jambo la kumshutumu Uhuru Kenyatta kwa ujanja linazidi kuudhi. Mtu huyu alijitolea kwa uwezo wake wote kwenye kampeni ya Azimio. Chini ya hali ngumu sana katika uwanja wake wa nyuma, alijitolea sana na kumkabidhi MHE Raila Odinga karibu kura milioni 1 kutoka Mlima Kenya. Ikiwa Nyanza Raila angepata kura 80%, kura za 200k katika mzozo zisingekuwa mjadala hivi sasa,” Njoroge alimtetea Kenyatta vikali dhidi ya matamshi ya Owino kumuita mwongo.

Vile vile ,Njoroge alitetea kutabasamu kwa Kenyatta kwa Ruto na kusema kwamba baada ya mahakama kudumisha ushindi wa Ruto, Kenyatta hakuwa na jinsi bali kukubali kuendesha kila kitu kama ambavyo katiba inamtaka ili kuhakikisha makabidhiano ya uongozi yanaenda kwa njia sahihi.