Fahamu gari lenye choo ndani rais wa Uganda Museveni anatembea nalo

Lina bafu yenye uwezo wa kupasha joto na hivyo kumpa Museveni fursa ya kuoga kwa maji baridi au moto

Muhtasari

• Jarida la Uganda Chimp Reports liliripoti kwamba Waganda wengi wanaliita gari hilo kama choo cha kutembea cha rais kwa vile huwa analitumia kwa haja zote akiwa nyanjani.

Gari lenye choo ndani la Museveni rais wa Uganda
Gari lenye choo ndani la Museveni rais wa Uganda
Image: Jonathan Manase//Facebook

Juzi katika halfa ya kuapishwa kwa rais William Ruto, wageni mbali mbali mashuhuri kutoka nje ya nchi walihudhuria hafla hiyo ya kihistoria

Kila mgeni alikuja kwa njia yake huku marais mbali mbali pia walijitoma katika jiji la Nairobi, lakini tukio moja lililoteka macho ya Wakenya ni rais wa Uganda Yoweri Museveni.

Rais huyo wa muda mrefu aliingia nchini akiwa amefuatwa na gari lake lenye kila kitu ndani kama nyumba kwa kimombo ‘Self Contained automobile vehicle’.

Jarida la Uganda Chimp Reports liliripoti kwamba Waganda wengi wanaliita gari hilo kama choo cha kutembea cha rais kwa vile huwa analitumia kwa haja zote akiwa nyanjani.

Wasichokijua ni kwamba gari hio ni zaidi ya choo cha kutembezwa. Gari hilo linalokadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya milioni 16 za Kenya, lina choo ndani, sehemu ya kupikia, sehemu ya kula, kitanda pamoja na jokofu lenye uwezo wa kuhifadhi lita 153 ya vinywaji mbali mbali.

Ndani pia mna bafu yenye uwezo wa kupasha joto na hivyo kumpa Museveni fursa ya kuoga kwa maji baridi au moto kulingana na chaguo lake.

Waandishi wa habari na wadau wa siasa wametafsiri kuwa Rais Museveni anafanya hivyo kwa ajili ya usalama wake.