Mwanasheria Ahmed Nasir ataka Matiang'i kushtakiwa kwa kufunga akaunti ya Twitter

Kulingana na Nasir, akaunti ya mtu anayehudumu serikalini si binafsi bali ni mali ya umma.

Muhtasari

• Kufuta au kufunga akaunti kama hizo bila mamlaka ya wazi ya serikali ni hatia inayosababisha kifungo cha jela au faini - Nasir.

Ahmed Nasir ataka Matiang'i kuchukuliwa hatua kwa kufunga Twitter yake
Ahmed Nasir ataka Matiang'i kuchukuliwa hatua kwa kufunga Twitter yake
Image: Twitter, maktaba

Mshauri mkuu wa kisheria Ahmed Nasir anataka aliyekuwa Waziri wa masuala ya ndani Dkt Fred Matiang’i kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa kuifunga akaunti yake ya Twitter.

Juzi baada ya rais William Ruto kuapishwa kama rais wa 5 wa kenya, Waziri Matiang’i ambaye alikuwa ni mkosoaji mkubwa wa sera za Ruto wakati wa kampeni zake aliifunga akaunti yake ya Twitter na siku mbili sasa hakuna taarifa zozote zilizotolewa kutokana na akaunti hiyo kutoweka mtandaoni ghafla.

Wakili Nasir sasa anasema kitendo cha Matiang’i kuifunga akaunti hiyo ni kinyume cha sheria na anafaa kuchukuliwa hatua. Mwanasheria huyo anadai kwamba akaunti ile ya Waziri Matiang’i ni ya umma na mtu ukiwa kama Waziri katika serikali akaunti zako zote za mitandaoni ni za umma na huwa zina baadhi ya taarifa zinazohusu umma kwa hiyo hufai kuifuta wala kuifunga isifikiwe na umma.

“Akaunti za Twitter zinazoendeshwa na Makatibu wa Baraza la Mawaziri kama vile Dkt Fred Matiang'i ni mali ya umma na zina habari ambazo ni za afisi anayoshikilia. Kufuta au kufunga akaunti kama hizo bila mamlaka ya wazi ya serikali ni hatia inayosababisha kifungo cha jela au faini,” mjuzi huyo wa sheria Ahmed Nasir aliandika kwenye Twitter.

Wengi walionekana kulizamia suala hilo na wengine kudai kwamab sheria kama hiyo haipo nchini Kenya kwani hata rais Kenyatta alifunga akaunti yake ya Twitter miaka kadhaa iliyopita kwa kile alisema wazi kwamba alishindwa kustahimili matusi kwenye mtandao huo unaotumiwa sana na Wakenya kujibizana vikali.