Pastor Ng'ang'a amtetea rais William Ruto kuhusu kudorora kwa uchumi

Ng'ang'a alisema rais anahitaji muda wa takriban miezi mitatu ya kutafuta namna ya kufufua uchumi.

Muhtasari

•Ng'ang'a ametoa wito kwa wakenya kumpa rais mpya William Ruto muda wa kuboresha uchumi unaoendelea kudorora.

•Pia aliwaomba Wakenya kutotilia maanani maneno ya wanasiasa huku akidai kuwa wengi wao ni wanafiki.

Muhubiri James Ng'ang'a
Image: WILFRED NYANGARESI

Mhubiri mwenye utata James Ng'ang'a ametoa wito kwa wakenya kumpa rais mpya William Ruto muda wa kuboresha uchumi unaoendelea kudorora.

Akiwahutubia waumini wa kanisa lake wakati wa ibada, Ng'ang'a alisema rais anahitaji muda wa takriban miezi mitatu ya kutafuta namna ya kufufua uchumi.

"Sasa mtu ambaye ameingia wiki moja tu atatoa pesa wapi, hata hajatangaza mawaziri wake," Ng'ang'a aliwaambia waumini.

Mtumishi huyo wa Mungu alibainisha kuwa hali ya sasa ya nchi inatokana na hatua za utawala ambao uliondoka.

"Mmepatie kama miezi tatu nne hivi ili aweze kutafuta mahali pesa ziliko na aweze kuteua mawaziri ili ajue jinsi atakavyoziba mashimo," alisema.

Aidha aliwaomba Wakenya kutotilia maanani maneno ya wanasiasa huku akidai kuwa wengi wao ni wanafiki. Alitoa mfano wa katibu mkuu wa COTU Francis Atwoli ambaye kwa sasa amebadilisha msimamo licha ya kumpinga Ruto wakati wa kampeni.

"Usije ukaamini wanasiasa, watakuuza na siku itakayofuata wanasalimiana," alisema.

Haya yanajiri huku Wakenya wakiendelea kulalamika kuhusu gharama ya juu ya maisha katika kipindi cha sasa. Wengi wamelalamika kuhusu ongezeko ya bei ya bidhaa kadhaa zikiwemo mafuta, unga na vyakula.

Hivi majuzi baadhi ya wanasiasa wanaoegemea upande wa serikali mpya waliibua madai kuwa rais ruto alipata Sh93,7 m pekee katika hazina.

"Uchumi hauko tena ICU Bali Kifo kwa sababu H.E Ruto alipata Sh93.7M pekee kwenye hazina, Uhuru alienda nyumbani na kila kitu. State Capture ni kweli !" Seneta wa Nandi Samson Cherargei alisema Jumamosi kupitia Twitter.

Aliongeza, "Nchi ni fukara, Wakenya kuweni na subira H.E Ruto atarekebisha hili kupitia mageuzi ya kiuchumi na Maombi kutoka kwetu sote. Amina."

Akiongea Jumanne wiki jana wakati wa kuapishwa kwake, Ruto alisema ruzuku ya mafuta imetumia pesa nyingi zisizo za lazima.

"Katika ruzuku ya mafuta pekee, jumla ya Ksh144 bilioniza walipa kodi zimetumika , ambayo ni Ksh 60 bilioni katika kipindi cha miezi 4 iliyopita," alisema.

Alisema mpango huo hauwezi kuendelea huku akitangaza kusitishwa  kwa ruzuku hiyo.