Tulizomewa katika mkutano wa IEBC huku Chebukati akitazama- Cherera adai

Cherera alisema hata hivyo baadhi ya wafanyakazi waliwashangilia.

Muhtasari

• Cherera amefichua kwamba alizomewa kwenye mkutano wa wafanyikazi wa tume hiyo uliofanyika Mombasa wiki jana.

•Alimkashifu Chebukati kwa kutofanya lolote wakati walipokuwa wakidhihakiwa na baadhi ya wafanyakazi.

wakati wa mkutano uliopita na wanahabari katika hoteli ya Serena.
Makamishna wa IEBC Justus Nyangaya, makamu mwenyekiti Juliana Cherera, Irene Masit na Francis Wanderi wakati wa mkutano uliopita na wanahabari katika hoteli ya Serena.
Image: REUTERS

Naibu mwenyekiti wa IEBC Juliana Cherera amefichua kwamba alizomewa kwenye mkutano wa wafanyikazi wa tume hiyo uliofanyika Mombasa wiki jana.

Wakati wa hafla hiyo, Cherera alisema makamishna wengine watatu waliojitenga na matokeo ya urais yaliyotangazwa na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati  mwezi jana pia walipata mapokezi mabaya.

Akithibitisha hali hiyo katika mahojiano na vyombo vya habari, Cherera alisema hata hivyo baadhi ya wafanyakazi waliwashangilia.

"Ndiyo, nilizomewa. Makamishna wengine walizomewa pia. Lakini katikati ya kuzomewa, wengine walitushangilia," Cherera aliambia NTV.

Naibu Mwenyekiti huyo alimkashifu Chebukati kwa kutofanya lolote wakati walipokuwa wakidhihakiwa na baadhi ya wafanyakazi.

“Mwenyekiti alikuwepo pale na alitazama kimya huku baadhi ya wafanyakazi wakituzomea na hakufanya lolote  kuwazuia,” aliongeza.

Hayo  yalitokea wakati wa mkutano wa tathmini ya baada ya uchaguzi mkuu  ambao ulifanyika mnamo Septemba 15.

Cherera na makamishna watatu wengine; Irene Masit, Francis Wanderi na Justus Nyang’aya walifanya kikao na wanahabari wakati ambapo Chebukati alipokuwa akimtangaza William Ruto kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais.