Uhuru ni rafiki yangu kwa miaka 20, nitamtafuta mambo yakitulia - DP Gachagua

Hatuna shida na rais wetu anayeondoka Uhuru Kenyatta - DP Gachagua

Muhtasari

• Gachagua alisema matamshi yake pindi baada ya kuapishwa hayakuwa yanamlenga kwa njia mbaya.

Rigathi Gachagua asema yeye na rais mstaafu Uhuru Kenyatta ni marafiki wakubwa
Rigathi Gachagua asema yeye na rais mstaafu Uhuru Kenyatta ni marafiki wakubwa
Image: facebook

Naibu rais Rigathi Gachagua amefunguka kwamba yeye hana tofuati zozote na rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Akizungumza katika mahojiano na runinga ya KTN usiku wa Jumapili, Gachagua alisema kwamba urafiki wake na Uhuru Kenyatta ni wa muda mrefu na atamtafuta wajiburudishwa kwa wakati mzuri pamoja.

 Alisema maneno ambayo alikuwa akiyazungumza dhidi yake ni siasa tu wala si uadui kama ambavyo wengi wamekuwa wakisema.

Naibu huyo wa rais alikuwa akijibu maswali kuhusu hotuba yake ya kwanza kama naibu rais Jumanne iliyopota ambapo alimrushia cheche kali rai mstaafu Uhuru Kenyatta.

“Hatuna shida na rais wetu anayeondoka Uhuru Kenyatta. Tunamtakia heri katika kustaafu. Unajua ni rafiki yangu wa miaka 20, na mambo yakitulia, nitamtafuta na kufurahia wakati mzuri na yeye,” Gachagua alisema.

Gachagua alisema kwamba rais mstaafu aliondoka na kuwarithisha deni kubwa la kitaifa pamoja na uchumi ulioporomoka vibaya mno.

 Wikendi baadhi ya viongozi kutoka kwa mrengo wa Kenya Kwanza waliibua madai kwamba hazina kuu ya serikali ya kitaifa ilikuwa na salio la milioni 93.7 pekee.

Matamshi ya Gachagua kwamba yeye hana uadui dhidi ya rais mstaafu si mara ya kwanza yanasikika kutoka kwa viongozi wa mrengo wa Ruto kwani rais pia aliwahi sikika mara kadhaa akisema kwamba hatokuwa na kinyongo dhidi ya Kenyatta licha ya kumtema na kuanza kumnadi Raila Odinga.