Mkosoaji wa Museveni, Stella Nyanzi atapeliwa Kenya kwa kuzimiwa gari alilokodisha

Nyanzi alisema alikodisha gari hilo kwa siku tatu kwa gharama ya 19600 ila likazimwa akiwa njiani.

Muhtasari

• Kenya ina wahuni wake! Leo, nimekubali kwamba kiwango cha ujambazi nchini Kenya ni safi - Nyanzi.

Stella Nyanzi akiwa amekwama kwenye gari hilo lililozima
Stella Nyanzi akiwa amekwama kwenye gari hilo lililozima
Image: facebook

Mkosoaji mkubwa wa uongozi wa rais wa Uganda Yoweri Museveni, mwandishi Stella Nyanzi amelalamika vikali kwa kufanyiwa utapeli akiwa nchini Kenya.

Nyanzi ambaye alisema kwamba alikuwa na kongamano la usomaji wa  kazi zake za fasihi katika jiji la Mombasa alikodisha gari na kulilipia ila alipokuwa njiani kuelekea Mombasa, mwenye gari lile alilizima kwa kufunga kifaa cha kufuatilia gari.

Nyanzi alilalama vikali kupitia kwa mitandao yake ya kijamii kwamba sasa ndio ameelewa utapeli nchini Kenya ni wa kiwango cha hadhi ya juu.

“Kenya ina wahuni wake! Leo, nimekubali kwamba kiwango cha ujambazi nchini Kenya ni cha juu, kimefuzu na kinahesabiwa kwa kiwango cha juu kuwadhalilisha watu wasio na hatia na kuwaacha  hoi,” Nyanzi alilalama.

Alisema gari hilo kubwa aina ya Voxy walikuwa wamelilipia kwa siku tatu ila mwenye gari aliamua kuwatapeli na baadae kufika hapo na kuwapokonya gari hilo na kuwaacha hapo wakiwa hoi.

“Tuliingia katika barabara ya Mombasa kabla jua halijatoka. Tulipofika tu Makindu, gari la kukodi lilisimama kabisa. Kila kitu kilikufa. Tulisukuma gari kando ya barabara, tukapata mafundi wawili wa eneo hilo kutoka Makindu ambao wote walithibitisha kuwa kifaa cha kufuatilia gari kilikuwa kimefunga gari. Tulimjulisha mwenyewe kwa jina David, ambaye alikataa kurejesha pesa zetu zilizolipwa ili kukodisha Voxy kwa siku tatu,” Nyanzi alielezea.

Alitudanganya kwamba alikuwa akitutumia gari lingine. Badala yake alikuja Makindu, akatuamuru tutoe vitu vyetu vya thamani kutoka kwenye gari lake, akazima kifaa cha kufuatilia gari, akaketi ndani na akaondoka kwa kasi kana kwamba yeye ndiye shetani. Tulibaki tukitazama,” aliongeza.

Alisema kutokana na  masaibu aliyokumbana nayo amelazimika kusitisha kongamano lake lilikuwa limeandaliwa kusoma kazi zake za ushairi na fasihi ya kiafrika.

Alisema kwamba walikuwa wamelipa ada zote kabla ya kukabidhiwa gari na walilipa gharama ya siku tatu pasi na kujua kwamba ndio mwanzo walikuwa wanawekwa kwenye kikaangio.

“Tulikodisha gari la Voxy  rangi ya kijivu KDC ***J kwa siku tatu kutoka Nairobi hadi Mombasa na kurudi. Tulilipa KES 6,500/= kwa kila siku maana kwa siku tatu tulimpa KES 19,600/=. Alisisitiza kulipwa kila kitu mapema,” Nyanzi alisema.