Naomba Ruto, Gachagua wanisaidie kumpata mwanangu - Mamake Mwenda Mbijiwe alia

Mwenda Mbijiwe ni mchanganuzi wa masuala ya usalama aliyetoweka kwa njia za utata miezi 15 iliyopita. Mamake bado ana imani yuko hai.

Muhtasari

• Ninawaomba wamrudishe mwanangu kwa sababu najua yu hai. Ikiwa angekufa, mwili wake ungeweza kugunduliwa muda mrefu uliopita - Jane Gatwiri.

Image: Maktaba, Screengrab

Mchambuzi wa masuala ya kiusalama Mwenda Mbijiwe alitoweka kwa njia za kutatanisha mnamo mwezi Juni mwaka jana ambapo mpaka leo hii hakuna habari yoyote imesikika kuhusu nani aliyemteka na alikopelekwa.

Mamake Jane Gatwiri sasa amejitokeza kwa mara nyingine tena akiulilia uongozi mpya wa rais Ruto na naibu wake Gachagua kufanya mchakato wa kumpata mwanawe – maiti ama mzima.

Jarida la Nation linaripoti kwamba Gatwiri anatarajia sasa serikali ya Ruto itatupa mwanga kwenye suala hilo la kutoweka kwa mwanawe kwani kionozi huyo kipindi cha kampeni alizungumzia mara si moja kuhusu kupotea kwa watu katika njia za utatanishi.

Mshauri huyo wa masuala ya usalama alitoweka mnamo Juni 12, 2021. Siku iliyofuata, gari alilokuwa amekodisha kwa wiki tatu kwa biashara liligunduliwa katika shamba la kahawa karibu na Tatu City, Kaunti ya Kiambu.

Jane Gatwiri katika mahojiano ya awali alisisitiza kwamba Imani yake inamtuma kuamini Mbijiwe bado yupo hai popote pale alipo hata kama hawajawahi kusikia kutoka kwake takribani miezi 15 sasa.

“Najua Rais Ruto na naibu wake Gachagua wanafahamu ninateseka. Mimi hulala mara chache na ninapoamka na ndoto mbaya, nikitetemeka. Ninawaomba wamrudishe mwanangu kwa sababu najua yu hai. Ikiwa angekufa, mwili wake ungeweza kugunduliwa muda mrefu uliopita,” Nation walimnukuu mamake Mbijiwe akisema kwa huzuni.

Mirzi minane iliyopita baada ya juhudi zote za kujaribu kupata ufumbuzi wa kupotea kwa Mbijiwe, ndugu yake aliamua kufanya kufuru kwa kuanza safari ya kutembea kutoka nyumbani kwao Meru hadi Nairobi kwa miguu ili kufika katika makau makuu ya upelelezi kupata majibu ya kutoweka kwa ndugu yake.

Familia hiyo sasa inaamini kwamba rais Ruto na serikali yake ndio msaada wa mwisho katika kuteua kitendawili cha kupotea kwa Mbijiwe ambaye mpaka sasa mazingira ya kutoweka kwake bado ni fumbo kubwa.