(+video) Martha Karua afurahishwa na klipu vijana walioigiza sauti yake na ya DP Gachagua

Karua alisema kwamab mwanadada aliyeigiza kama yeye aliipata barabara.

Muhtasari

• Huyo wa kuigiza kama Martha Karua alifanya vizuri kweli kweli - Karua aliandika Twitter.

Kinara wa chama cha Narc Kenya Martha Karua ameshabikia klipu inayosambazwa mitandaoni ikiwaonyesha wachekeshaji wawili wakiigiza sauti za Karua na naibu rais Rigathi Gachagua.

Klipu hiyo iliyofanywa na mwigizaji wa ucheshi KK Mwenyewe inamuonesha akichukua nafasi ya naibu rais Rigathi Gachagua na mwanadada mmoja akiigiza kama Martha Karua.

Wawili hao wanaigiza kukutana kwa mara ya kwanza kwa Karua na Gachagua, tangu tangu mahakama ya upeo kutupilia mbali ombi la muungano wa Azimio la Umoja One Kenya ambako Karua alikuwa naibu mpeperusha bendera.

Wawili hao wanakutana na kujibizana vikali kuhusu matokeo ya uchaguzi huku KK Mwenyewe ambaye anaigiza kama naibu rais akitumia misemo kwamab wao kama Kenya Kwanza walimtegemea Mungu na ndiye aliyewapa ushindi.

Mwanadada huyo anachukua nafasi ya Karua naye anamjibu vikali kwa lafudhi nzito ya Kikuyu kwamba Ruto na mwenyekiti wa tume huru ya mipaka na uchaguzi IEBC Wafula Chebukati walifanya njama ya kuibia Azimio kura.

Klipu hii ilipakiwa na kusambazwa mitandaoni ambapo wimbi hilo lilimfikia Karua amabye bado ako katika hali ya kusherehekea miaka 65 ya kuzaliwa.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Karua alisema kwamba mwanadada huyo aliigiza kama yeye vizuri ajabu na kumhongera.

“MK (Martha Karua) aliigiza vizuri kabisa,” Karua aliandika kwenye Twitter akiinukuu video hiyo iliyopakiwa na mtumizi mmoja kwa jina Patrick Gachagoh.