Wasiliana na wakili wangu kabla nifike - Miguna awaambia Matiang'i, Kibicho

Miguna aliwataka watatu hao kutii uamuzi wa mahakama kumfidia hasara zote kabla atue nchini.

Muhtasari

• Kwa Fred Matiang'i, Karanja Kibicho na Gordon Kihalangwa: Mmeagizwa kuwasiliana na wakili wangu, Adrian Kamotho Njenga na mtatue masuala yote kabla nifike - Miguna.

Miguna Miguna ataka Matiang'i na wenzake kumfidia kabla hajatua nchini
Miguna Miguna ataka Matiang'i na wenzake kumfidia kabla hajatua nchini
Image: Maktaba

Usiku wa Alhamis wakili aliyeko uhamishoni Canada Miguna Miguna alitangaza kwamba hatimaye amepata hati ya usafiri kurudi nyumbani baada ya kukabidhiwa pasipoti yake.

Kabla ya kurudi kwake, Miguna Miguna ameanza kutema moto kwa baadhi ya watu anaosema walikuwa mstari wa mbele kumfurusha nchini na pia kuharibu pasipoti yake.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Miguna kama kawaida yake amekuwa akiachia mwendelezo wa maneno hayo ambapo sasa amelenga kwa Waziri wa usalama wa ndani anayeondoka Dkt. Fred Matiang’i, katibu katika wizara hiyo Karanja Kibicho na aliyekuwa msimamizi katika idara ya uhamiaji Gordon Kihalangwa.

Aliwataka watatu hao kufanya hima ili kuwasiliana na mawakili wake ili kufanya marekebisho na ukarabati wa vitu vyake vyote vilivyoharibiwa wakati anafurushwa nchini mapema 2018 kwa fujo.

Aliwataka kufanya hivo hima kabla hajarudi ili kujihakikishia amani.

“Kwa Fred Matiang'i, Karanja Kibicho na Gordon Kihalangwa: Mmeagizwa kuwasiliana na wakili wangu, Adrian Kamotho Njenga, na kutatua HASARA na GHARAMA ambazo Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani ilinipatia katika kesi mbalimbali nilizoshinda tangu 2018. Fanya hivyo mara moja KABLA sijatua,” Miguna aliandika.

Wakili huyo alienda kwenye mitandao ya kijamii kutangaza kuwa Rais William Ruto alimpa pasipoti mpya. Katika chapisho lake la mtandao wa kijamii, Miguna alisema sasa anasubiri kuondolewa kwa vizuizi vyekundu ambavyo vilimzuia kusafiri mara kadhaa kuja nchini.

"Rais William Samoei Ruto ameniletea mpya. Sikuhitaji kutia sahihi fomu za kipumbavu walizokuwa wakizungumzia. Nasubiri kuondolewa kwa vizuizi vyekundu," alisema.