"Hivi ndio mlipotosha Uhuru" Sudi amzomea Ngunyi kwa kumshauri Gachagua

Ngunyi alikuwa anatoa ushauri kwa Gachagua kwamba asifanye kazi sana kumzidi bosi wake.

Muhtasari

• Tumejikita katika utoaji wa huduma na wala hatubabaiki na madaraka - Sudi.

Sudi ajibizana vikali na Ngunyi
Sudi ajibizana vikali na Ngunyi
Image: Twitter

  Ni wiki moja sasa tangu rais William Ruto kuondoka nchini kuhudhuria hafla mbali mbali katika mataifa ya Uingereza na Marekani na muda huu wote taifa limekuwa likiendeshwa na naibu wake Rigathi Gachagua.

Kwa kweli Gachagua amekuwa akionekana kupiga azi kutoka kufungulia rasmi mbolea ya bei rahisi kwa wakulima hadi kuwakilisha rais katika hafla ya muziki jijini Kisumu ambako alienda na ndege ya jeshi la wanahewa.

Hatua hii ya uchapakazi wa naibu rais imewatia tumbo joto baadhi ya wachanganuzi wa masuala ya kisiasa ambao wanahisi ni kama anafanya kazi ili kuonesha umahiri wake kushinda mkuu wake – rais William Ruto.

Mutahi Ngunyi ambaye alikuwa mwandani wa karibu wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta alimshauri Gachagua kupitia Twitter kwamba asijifanya kimbelembele kujionesha anajua kuchapa kazi sana kumshinda bosi wake na kuonya kwamba hilo litamgharimu.

Kulingana na Ngunyi, naibu hafai kuchapa kazi kumshinda mkubwa wake ambaye ni rais kwa sababu kiti cha urais ni kimoja chenye wivu sana.

“Mpendwa Riggy G. SHERIA ya Kwanza ya MADARAKA: Usimzidi bosi wako. Ulifanya hivi Siku ya Uzinduzi. Na leo UMERUKA kwa NDEGE ya kijeshi hadi Kisumu ukiwa umevaa miwani. Nchi iliipenda. Lakini kumbuka hili kutoka kwa Arap Moi COOKBOOK of SIASA: Urais ni taasisi yenye WIVU,” Ngunyi aliandika kwenye Twitter.

Hili halikuenda vizuri na baadhi ya wanandani wa naibu rais pamoja pia na rais Ruto. Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi aliingia kwenye mitandao ya kijamii na kutema moto kwa Ngunyi huku akimwambia kwamba huu ndio ushauri wa kupotosha waliompa rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

“Hivi ndivyo mlivyompotosha Uhuru Kenyatta wakati wa uongozi wake. Tumejikita katika utoaji wa huduma na wala hatubabaiki na madaraka. Rigathi Gachagua ndiye Naibu Naibu Mchapakazi bora zaidi kamwe usijali kumuona juu ya gari au ndege ya kijeshi. Huo ujinga ndio mlimfanya Uhuru akapoteza mwelekeo,” Oscar Sudi alimpiga bomu la moto Ngunyi.

Bado inasubiriwa kuona kama Ngunyi atajibu mipigo ama atanywea na kukubali kupigwa bomu hilo zito! wiki mbili sasa tangu kuondoka kwa rais