Mwenyekiti wa Gor mahia, Rachier afichua jinsi alijiunga na Freemason, "Sikutoa kafara"

Wakili huyo alisema yeye anamshukuru Mungu watoto wake wote wako hai na hakuwahi kushrutishwa kutoa kafara ili kujiunga.

Muhtasari

• Alisema katika kundi hilo wanachama wanatoka katika dini zote na wala hawabagui.

• Pia alisema wako na madaktari wakubwa, mawakili na watu wengine wenye majina ya kutajika.

Mwenyekiti wa Gor Mahia Ambrose Rachier afichua amekuwa mwanachama freemason kwa miaka 28.
Mwenyekiti wa Gor Mahia Ambrose Rachier afichua amekuwa mwanachama freemason kwa miaka 28.
Image: MAKTABA

Wikendi iliyopita kituo kimoja cha runinga humu nchini kilipeperusha Makala yenye ukakasi kuhusu shirika la ushirikina la Freemason.

Katika Makala hayo, wakili ambaye pia anajiongeza kama mwenyekiti wa timu ya soka ya Gor Mahia, Ambrose Rachier alizungumza na kuweka wazi kuwa yeye ni mmoja wa wanachama katika kundi hilo linalodhaniwa kujihusisha na kafara za kishetani.

Rachier alifunguka mengi kwa mapana na kukosoa dhana mbali mbali zilizopo vichwani mwa watu kuhusu kundi la Freemason, si tu humu nchini bali kote duniani.

Mwenyekiti huyo alisema Freemason si kundi la kishetani kama ambavyo wengi wanalichukulia kwani pia wao husoma maandiko matakatifu na katu hawalifanyii jina la Mungu au mwanawe Yesu mzaha.

“Ukifika kwenye jumba la Freemason, jambo la kwanza unalopata ni nukuu ya Mfalme Sulemani kwa Mungu. Nadhani wengi wanazungumza kwa mtazamo wa Ukristo, lakini Freemason haitokani na dini fulani,” Rachier alisema.

Alisema kundi hilo halibagui mtu kutoka dini yeyote kwani miongoni mwao kuna Wakristu, Waislamu na hata wale wasiomwamini Mungu hata kidogo.

“Tuna Waislamu katika freemason, Wakristo, Wabudha na wachache wasioamini Mungu, hivyo hakuna rejea yoyote kwa masuala ya ibada ya shetani, shetani ni nani," alisema Rachier.

Vile vile, Rachier alikanusha dhana kwamba mtu akiingia kuwa mwanachama ni sharti atoe kafara ya damu ya mtu. Alisema yeye alijiunga bure bila kutoa kafara ya mwanawe au mtu wake wa akribu hata mmoja.

"Nataka kumshukuru Mungu kwa hili. Watoto wangu wote wako hai. Sijapoteza ndugu wala mtoto, na wanajulikana," alifichua huku akisema amekuwa mwanachama kwa miaka 28 sasa.

Pia alizungumzia suala la kundi hilo kuwafanya wanachama kuwa maarufu na matajiri. Rachier alisema azimio kubwa la kundi la Freemason si kuwafanya watu matajiri bali kazi yao ni kama kutoa msaada tu kwa wanajamii ili kuwaboreshea maisha.

“Watu wengi huko ni Wakenya wa kawaida tu. Baadhi yao ni wafanyabiashara, wengine ni madaktari na wanasheria. Sidhani kama tuna wanasiasa. Dhana ya kawaida sio utajiri ni mazoea ya hisani,” Rachier alifunguka kwa ukakasi mkubwa.