Dereva wa lori anusurika kifo baada ya kuvamiwa na majambazi

Mwaura alinusurika tukio hilo baada ya kujiokoa kwa kupigana

Muhtasari

•Majambazi hao waliokuwa kwenye gari aina ya Probox, walimvamia katika eneo la Kamandura kwenye barabara kuu ya Nairobi- Nakuru.

•Dereva huyo ambaye jina lake ni Mwaura aliamua kujisalimisha kwa mikono ya majambazi hao ila akaamua kujitetea kwa vita.

Pingu
Image: Radio Jambo

Kitengo cha upelelezi wa jinai na uhalifu kimetangaza kuwa dereva mmoja alivaamiwa na majambazi watatu ambao baadaye walimpa majeraha.

Imeripotiwa kuwa dereva huyo alijikuta katika hali hiyo wakati genge la wezi lilipomvamia mwendo wa saa tisa asubuhi alipokuwa akiendesha lori lake.

Dereva huyo alikuwa ametoka katika eneo la Potato Rich Highlands huko Molo akielekea Kajiado alipovaamiwa na majambazi hao.

Majambazi hao waliokuwa kwenye gari aina ya Probox, walimvamia katika eneo la Kamandura kwenye barabara kuu ya Nairobi- Nakuru. Dereva wa gari la majambazi aliendesha kwa kasi na kuenda mbele ya lorI hilo ili kumzuia dereva huyo na safari yake.

"Majambazi wawili walikuwa wakibembea kwenye mlango wa gari na kurukia barabarani ndipo wakaelekea kwenye lorry hilo," Kitengo cha upelezi wa uhalifu wa jinai kilisema kupitia mtandao wa Twitter.

Majambazi hao walimtishia dereva huyo na kumpa chaguo mbili ambapo dereva huyo alikuwa ajisalimishe kwao ama awaachie lori hilo.

Dereva huyo ambaye jina lake ni Mwaura aliamua kujisalimisha kwa mikono ya majambazi hao ila akaamua kujitetea kwa vita.

Aliwarushia majambazi hao wawili mateke yaliyowaangusha chini na kuwabingirisha mpaka kwenye lami.

Jambazi wa tatu alijipata kwenye kinyanganyiro hicho na kushtukia amepigwa ngumi iliyomrusha mita chache mbele ya lori.

"Ndipo Mwaura akatoroka kuenda kwa usalama wake, akaelekea kwenye kituo cha petroli cha Rubis iliyokuwa mita 100 mbele ya tukio hilo," kitengo hicho kilisema.

Kabla ya Mwaura kupata pumziko, jambazi mmoja alijitokeza na kumdunga kisu kwenye mguu wake wa kulia.

Alichokumbuka Mwaura ni kuwa aliskia majambazi hao wakiulizana ikiwa wamekutana na kumvamia mtu aliyerukwa na akili.

Majambazi hao walitoweka na lori ila Mwaura alisaidiwa na  mlinzi  aliyemsaidia kuripoti tukio hilo. Mlinzi huyo aliripoti tukio hilo kwa polisi wa Tigoni baada ya kupewa maelezo kuhusu lori hilo ndipo mapolisi wakaanza kulitafuta lori hilo.

Baadaye mapolisi walikutana na lori hilo lililokuwa likiendeshwa na jambazi mmoja na kulisimamisha. Hata hivyo, majambazi hao hawakusimamisha lori hilo ila walishukia mbele na kuliwacha lori hilo kuingia kwenye mtaro kabla ya kutorokea vichakani.

Maafisa waliweza kumkamata mmoja wao anayejulikana kama Alexander Mwaniki, walipotifua risasi baada ya jaribio lao la kulihepa lori hilo ili lisiwakanyage.

"Wengine walitoweka na kutorekea pasipojulikana huku mwenzao mmoja ambaye sasa ni mshukiwa akihojiwa na kujibu mashataka kuhusu wizi wa kimabavu huo. Wakati huo huo, lori hilo liliegeshwa kwenye stesheni ya ofisi ya polisi huku dereva akipokea matibabu kwenye hospitali ya Tigoi," ujumbe huo wa kitengo hicho ulisema.

Polisi bado wanaendelea kuwatafuta majambazi hao wengine waliotoroka na majeraha yaliyosababishwa na mtutu wa bunduki.