Umaskini ulinifanya nivae shati la baba yangu - Mkewe Gachagua

Wanjiku aliwahimiza wanawake kufanya kazi kwa bidii na kamwe wasiruhusu maisha yao ya nyuma yafafanue maisha yao ya baadaye.

Muhtasari
  • Hazina ilitenga Sh502 milioni kwa afisi za Mke wa Rais na ofisi ya Wanjiku katika mwaka wa kifedha ulioanza Julai 1
mama Dorcas Gachagua amesema yeye atawapa watoto wa kiume kipaumbele zaidi
mama Dorcas Gachagua amesema yeye atawapa watoto wa kiume kipaumbele zaidi
Image: Maktaba

Mkewe naibu rais Dorcas Wanjiku Gachagua ameweka wazi masaibu aliyopitia alipokuwa akilelewa katika mitaa ya mabanda ya Kiandutu mjini Thika.

Wanjiku alikuwa akihutubia kundi la wasichana wakati wa uzinduzi wa programu ya Jamii Femmes na Wakfu wa Coca Cola mnamo Oktoba 14.

Takriban wanawake 2,100 wa Kenya katika biashara walikuwa wamekusanyika kwa ajili ya mafunzo ya ujuzi wa kifedha na ujasiriamali.

Huku akiwahimiza wasichana hao kutokata tamaa katika ndoto zao, alisimulia jinsi alivyolelewa na mjane kufuatia kufariki kwa babake akiwa bado mdogo.

"Nimejua jinsi ya kuwa na njaa, ninajua kutokuwa na nguo. Nilikuwa nikivaa shati la baba kuanzia Jumatatu hadi Jumapili," alisema.

Hali ilikuwa mbaya sana hivi kwamba mara kwa mara  Wanjiku angekaa bila nguo.

"Ningeenda mtoni, nikanawa, nikakaa uchi na kusubiri ikauke. Kwa hiyo, naweza kuhisi na kutambua matatizo ya wengine," alisema.

Wanjiku sasa ni ushuhuda unaotembea wa mwanzo mnyenyekevu. Anatembea na timu ya wafanyakazi wa usalama na madereva.

"Kabla ya watu kuniita Mheshimiwa, mimi ni mama wa watoto wawili, nilizaliwa na mjane, na nina ndugu nane," alisema.

Wanjiku aliwahimiza wanawake kufanya kazi kwa bidii na kamwe wasiruhusu maisha yao ya nyuma yafafanue maisha yao ya baadaye.

“Ukimwezesha mwanamke, umetajirisha jamii nzima. Wanawake wanaweza kumfundisha binadamu mzima jinsi ya kuzungumza, kutembea, kukaa na hata kula,” alisema.

Wanjiku, ambaye ni mchungaji, sasa ni mke wa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Hazina ilitenga Sh502 milioni kwa afisi za Mke wa Rais na ofisi ya Wanjiku katika mwaka wa kifedha ulioanza Julai 1.

Ofisi ya Wanjiku ilitengewa Sh242 milioni zitakazotumika kulipa mishahara ya wasaidizi wao na kwa kiasi kikubwa, gharama zao za usafiri na burudani.