Museveni akaa mbali na mwanahabari wa Kenya wakati wa mahojiano, picha yazua vichekesho

Wengine walisema kwamba anaogopa kukaribiana na mwanahabari kutokana na tishio la Ebola au Corona.

Muhtasari

• “Tofauti kati ya hii na mazungumzo ya simu ni kwamba mnaonana moja kwa moja,” mwingine alisema.

Museveni akaa mbali na mwanahabari wakati wa mahojiano
Museveni akaa mbali na mwanahabari wakati wa mahojiano
Image: Instagram

Mwanahabari wa runinga Sophia Wanuna amewachekesha wanamitandao baada ya kupakia picha moja inayoonesha mahojiano yake na rais wa Uganda, Yoweri Museveni.

Katika picha hiyo, Wanuna na rais Museveni wanaonekana wameketi nje kwenye mandhari mazuri yenye mvuto wa aina yake.

Wawili hao ambao walifanya mahojoano ya kipekee chini ya mti walionekana kuketi mbali kabisa kutoka kwa mwingine, jambo ambalo limewachekesha wanamitandao ambao wameona picha ile.

Mwanahabari Wanuna anaonekana akiwa ameketi upande wa kulia chini ya mti akiwa na kipaza sauti chake huku upande wa kulia, mita kadhaa mbali naye ameketi rais Museveni ambaye amejipanga vilivyo na vinywaji vyake juu ya kimeza kidogo kando yake na kipaza sauti mbele yake pia.

“Umbali wa kimwili kwa ubora wake 🤣🤣 Moja kwa mmoja na Rais wa Uganda @kagutamuseveni,” Wanuna aliandika kwa utani.

Umbali huu uliwashangaza na kuwachekesha wengi huku baadhi wakisema kwamba huenda rais huyo aliamua kujitenga mbali kutokana na tishio la janga la Corona ambalo kwa mara nyingi limekuwa likisemekana kuwashambulia kwa urahisi watu wenye umri uliosonga kama wake.

Wengine walisema ni kutokana na ugonjwa wa Ebola ambao uko nchini Uganda na ambao unazidi kupenyeza kwa kasi ya ajabu nchini humo.

Aidha, kunao wengine ambao walizua utani kuhusu umbali huo wao huku wakitaka kujia hayo mahojiano yalifanyika aje au walikuwa wanapigiana kelele ilmradi kusikika na mwingine.

“Uliwezaje hata kumsikia?” Aliuliza mwanahabari mwenza Yvonne Okwara.

“Hata hiyo ni afadhai kidogo, wengine hukaa mbali naye mara mbili zaidi ya hapo,” Joy Doreen Biira aliandika.

“Piga hesabu ya umbali kati ya mwanahabari Wanuna na rais Museveni, bila kutumia kikokotoo,” alitania mtangazaji Mwende Macharia.

“Tofauti kati ya hii na mazungumzo ya simu ni kwamba mnaonana moja kwa moja,” mwingine alisema.