Tayari mshahara wa mwezi jana umeisha, SRC msikate tena tafadhali - MP Salasya alia

Mbunge huyo aliitaka tume ya kuratibu mishahara na marupurupu kutopunguza mishahara ya wabunge kwani tayari wanachokipata hakiwatoshi.

Muhtasari

• Alisema mshahara wake mwingi uliisha wikendi iliyopita ambapo alisema alikuwa na shughuli nyingi.

Mbunge Salasya asema mshahara hautoshi
Mbunge Salasya asema mshahara hautoshi
Image: Twitter

Mbunge wa Mumias East Peter Salasya kwa mara nyingine amekuja na gumzo jipya, safari hii akilia kuhusu mshahara ambao wabunge wanapata.

Akizungumza katika sehemu ambayo hafla ya msiba wa mamake gavana wa Kakamega, Fernandes Barasa itafanyika, alisema kwamba wiki ambayo imepita ilikuwa ngum kwake kwani alitumia pesa zake nyingi katika kukimu mahitaji mbalimbali ya watu wa eneobunge lake.

Mbunge huyo ambaye ni mzungumzaji sana alitoa onyo kwa tume ya kuratibu mishahara na marupurupu, SRC dhidi ya mpango wao wa kutaka kupunguza mishahara ya wabunge.

Alisema kwamba tayari mshahara wanaopata hautoshi kwani kwa mfano mshahara wake wa mwezi jana uliisha wiki iliyopita.

“Hii wikendi imepita imekuwa na matukio mengi sana kwangu waah. Halafu SRC wanafikiria kuchuja mshahara wa wabunge, itakuwa ni hujuma kubwa sana, hata mshahara wa mwezi jana uliisha kitambo,” Peter Salasya aliandika kwenye Twitter yake.

Mbunge huyo alisema ameanza kuweka mikakati ya kukutana na makundi mbalimbali katika jamii wakiwemo vijana, kina mama na wazee ili kuwasikiliza kile ambacho wanakitaka na kutathmini njia ya kuwafanyia kazi.

Baadhi walimsuta kwa kuanza kulalama kuhusu mshahara hali ya kuwa walimchagua pasi na chochote. Walimshauri kukoma kulalama na badala yake kuanza kufanya kazi kwani tayari muda wake wa miaka mitano ushaanza kutiririka.

“Tulikuchagua pasi na kitu chochote, umeanza kulalama hapa na pale. Punguza kupiga sherehe, fanya kazi nanii kwani miaka yako 5 imeanza kuhesabiwa usiseme sikukwambia,” Enock Mwanza alimshauri.

“SRC iko sahihi. Infact ningekuwa mimi ningesema wabunge walipwe kima cha chini cha mshahara. Nyie mnaamini Wakenya wa kawaida wanaweza kuishi kwa vitu kama hivyo. Kisha unapaswa kuongoza kutoka mbele. Hukuwekwa ofisini kwa sababu ya ushabiki sivyo? Unajisahau kaka,” James Mwadeghu alisema.