Nyani ahudhuria msiba wa mwanaume aliyekuwa anampa chakula na kumbusu usoni

Nyani huyo alionekana akilia kwikwi huku akimpapasa marehemu usoni

Muhtasari

• “Ni kweli, wanyama pekee ndio huwa na upendo wa kweli bila vigezo vyovyote,” mmoja alisema.

 

Upo msemo unaosema kuwa, unaweza ukamlisha binadamu kwa miaka kumi lakini akakusahau kwa siku moja, vile vile unaweza ukamlisha mnyama kwa siku moja akakukumbuka kwa miaka 10 – bila shaka, huenda kuna ukweli usiomithilika!

Nchini Sri Lanka, kisa cha kushangaza kilishuhudiwa wakati nyani alihudhuria mazishi ya mkulima mmoja ambaye alikuwa anapenda kumpa chakula enzi za uhai wake.

Mwanaume huyo marehemu kwa jina Peetambaram Rajan, 56, aliripotiwa kufariki baada ya kupata ugonjwa wa ghafla katika nyumba yake ya msituni huko Batticaloa, Sri Lanka.

Lakini katika maisha yake yote, alijulikana kwa kulisha tumbili-mwitu kila siku kwa matunda na biskuti kwani wawili hao walianzisha uhusiano wa karibu sana.

Video iliyosambaza mitandaoni na ambayo ilipakiwa na shirika moja la habari kwenye Twitter kwa jina News First, nyani huyo anaonekana akihudhuria msiba wa mzee huyo na hata kubusu mwili wake katika panda la uso.

Nyani huyo aliyeonekana kulemewa na hisia juu ya jeneza la mzee huyo alilazimika kuondolewa pale na waombolezaji wengine huku akikataa kabisa kuamini kama rafiki yake aliyekuwa anamlisha ndio mwanzo anafukiwa kabisa wasionane tena.

“Nyani aomboleza kifo cha mwanaume ambaye alikuwa anamlisha matunda,” News First waliripoti kwenye Twitter.

Watu mbali mbali walishangazwa na kitendo hicho cha nyani na kukitaja kama upendo wa kweli ambao hauna mipaka wala vikwazo.

“Ni kweli, wanyama pekee ndio huwa na upendo wa kweli bila vigezo vyovyote,” mmoja alisema.

“Najua kwa kweli mke wangu hatahudhuria mazishi yangu,” mwingine alizua utani ambao una uchungu ndani yake.