Winnie Odinga asherehekea marehemu kakake Fidel kufikisha miaka 49

Winnie alimkumbuka kakake katika chapisho hilo huku akipakia picha yao zamani wakiwa wadogo.

Muhtasari

• Fidel alikufa mnamo Januari 4, 2015, baada ya mapumziko ya usiku. Alipatikana katika hali ya kutojielewa katika nyumba yake huko Karen.

Winnie amkumbuka Fidel
Winnie amkumbuka Fidel
Image: Instagram

Kitinda mimba wa kinara wa ODM Raila Odinga, Winnie Odinga Jumatano alimkumbuka marehemu kakake Fidel Odinga katika chapisho la kuliza.

Kupitia instastory yake, Winnie alimsherehekea Fidel na kusema kwamba angekuwa hai angekuwa anafikisha miaka 49, na kusema kwamba kila mtu katika familia yake anakosa furaha, tabasamu na uchangamfu wake enzi za uhai wake.

“Hii ingekuwa siku yako ya kufikisha miaka 49. Pumzika kwa Amani baba Ally,” Winnie aliandika katika chapisho hilo lililokuwa na hisia nyingi.

Alipakia picha ya Fidel ya zamani akiwa na yeye enzi za udogo wao. Fidel Castro alikuwa amevalia sare ya kijivu ya shule huku Winnie akiwa katoto kando yake akiwa amevalia nguo ya bluu.

 Miezi michache iliyopita alikuwa anazungumza na Mwafreeka ambapo alifunguka kwamba wakati ndugu yake alifariki mnamo mwaka 2015, hakulia hata kidogo ila baadae ndio alikuja kukumbwa na msongo wa mawazo na unyongovu mkubwa.

“Alipofariki sikulia. Nilianza kulia tu kama tulipokuwa tunamzika. Wakati wa kufanya mchakato wa mazishi, watu wengi wako karibu, haujisikii, ni baada ya mwili huo kuingia na uko tu na familia yako ndipo unapohisi. Hapo ndipo watu wanaingia kwenye mfadhaiko,” Winnie alisema.

Fidel alikufa mnamo Januari 4, 2015, baada ya mapumziko ya usiku. Alipatikana katika hali ya kutojielewa katika nyumba yake huko Karen. Winnie kila mara kwa mara, amezungumza kuhusu marehemu kaka yake.

Mwanadada huyo mwenye umri wa miaka 32 anasema siku zingine yuko sawa, siku zingine inamhuzunisha au anaweza kuanza kulia.

"Mchakato wa huzuni ni tofauti kwa kila mtu. Jambo la muhimu zaidi ni kuhuzunika, usijifanye kama haipo, njia pekee ya kutoka ni kuipitia, "alisema.