Fahamu unahitaji nini ili kupata mkopo wa Hustler Fund

Kuingia katika hati kiapo cha kukubali kufungwa jela endapo utakosa kurudisha pesa hizo ni miongoni mwa vigezo.

Muhtasari

• Kikundi chenu lazima kifungue akaunti katika benki ya KCB au National

Kuanzia mwezi Desemba tarehe mosi, serikali ya rais William Ruto itazindua utoaji wa hela ya kuwawezesha watu wa chini kutusua kibiashara almaarufu Hustler Fund.

Lakini je, unajua jinsi ya kupata pesa hizo na ni vigezo vipi unafaa kuwa navyo ili kupata mkopo huo kutoka kwa serikali?

Hapa tunakuandalia baadhi ya vigezo unavyohitaji kuafikiana navyo wewe kama ‘Hustler’ mwenye mawazo na fikira za kuanzisha biashara yako kupitia pesa hizo zitakazotolewa kwa njia ya mikopo.

  • Mwanzo lazima uwe katika kikundi cha vijana au kina mama
  • Katika kikundi chenu hicho, muwe na pendekezo kwa njia ya maandishi kuonesha jinsi mnapanga kuratibu matumizi ya pesa hizo.
  • Muwe na cheti cha maadili mema kutoka kwa idara ya upelelezi wa jinai na uhalifu DCI.
  • Kikundi chenu sharti kiwe na anwani inayoonesha mahali biashara yenu itakuwa ikifanyiwa.
  • Lazima muwe na sahihi kutoka kwa wadhamana 4, wawili kati yao sharti wawe kutoka familia yako ama mnahusiana kinasaba.
  • Ni sharti muingie katika miadi na serikali katika makubaliano kwa njia ya sahihi kutofichua makubaliano yoyote na pia kukubali kufungwa jela kwa muda utakaotajwa endapo utakwepa kuilipa serikali pesa hizo ndani ya miezi 6.
  • Muwe na akaunti ya benki katika tawi lolote la benki ya National au KCB pekee.
  • Mtoe cheti cha kulipa ushuru kutoka KRA.

Ingawa awali alikuwa amewatangazia Wakenya kwamba pesa hizo zingegawanywa kama mikopo, si ruzuku, Rais Ruto baadaye alisema,

“Si pesa za bure; ni pesa za biashara utakazorejesha…Tunataka kuhakikisha kuwa Wakenya hawawi mawindo ya watu wanaotoza riba kubwa sana kwa mikopo.”