"Hatuhitaji ushauri wako" DP Gachagua azidi kumshambulia Raila Odinga

Hivi majuzi gavana Orengo alimkomesha Gachagua dhidi ya kuendelea kumshambulia Odinga lakini ni kama DP ndio mwanzo ananoa kisu chake.

Muhtasari

• Wewe mzee wa upinzani, ulikuwa rais mwenza kwa Uhuru Kenyatta. Mambo yote unayotuambia tufanye, ulikuwa na miaka 5 na Kenyatta kuyatekeleza - Gachagua.

DP azidi kumshambulia Odinga vikali
DP azidi kumshambulia Odinga vikali
Image: Facebook

Naibu rais Rigathi Gachagua kwa mara nyingine amekiuka matakwa ya baadhi ya viongozi kutoka mrengo wa upinzani waliomtaka kukoma kumzungumzia kinara wao Raila Odinga na badala yake kuwafanyia wananchi kazi.

Gachagua ambaye Jumamosi alikuwa katika kaunti ya Kajiado akiongoza shughuli ya kusambaza vyakula vya msaada kwa waathirika wa ukame alizidisha mishale yake dhidi ya Odinga huku akimtaka kukaa mbali na serikali ili kujionea jinsi uongozi unaendeshwa.

Naibu rais huyo ambaye ni mwenye misimamo mikali alisema kwamba Odinga hana wajibu wowote wa kuiambia serikali ya Kenya Kwanza kile cha kufanya kwani alikuwa ndani ya serikali ya Jubilee kwa miaka karibia mitano na hakutekeleza mambo hayo.

Alimtetea rais Ruto kwamba afisa wote wa polisi waliohusika katika kupotea kwa baadhi ya rais kwa njia za utata ni sharti watachukuliwa hatua, suala ambalo juzi Odinga alionekana kupinga kwa kile alisema kwamba Ruto ameingiza siasa za kulipa kisasi katika kuwahukumu maafisa hao na pengine analenga kuwashawishi kumtia hatiani aliyekuwa mkuu wa DCI, George Kinoti.

“Na tungetaka kuwaambia nyinyi watu wa upinzani, achana na William Ruto afanye kazi. Wewe mzee wa upinzani, ulikuwa rais mwenza kwa Uhuru Kenyatta. Mambo yote unayotuambia tufanye, ulikuwa na miaka 5 na Kenyatta kuyatekeleza, na hukufanikiwa. Wewe kaa nyumbani uangalie vile Kenya inaongozwa. Sisi hatuna nafasi na wewe, hatukuhitaji katika serikali yetu, hatuhitaji ushauri wako,” Gachagua alisema kwa ukali.