Gavana Natembeya ampongeza muuguzi aliyeburudisha mtoto mgonjwa

Gavana huyo kupitia ukurasa wake wa Twitter alisifu kazi ya muuguzi huyo aliyetambuliwa kama Elizabeth Robai

Muhtasari
  • Lukelesia alichangamsha mioyo ya Wakenya wengi mtandaoni ambao walithamini jitihada zake za kuweka tabasamu kwenye uso wa mtoto huyo
gavana george natembeya
Image: hisani

Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya ametambua shauku ya muuguzi anayevuma kwenye mitandao ya kijamii kwa ajili ya kuburudisha mtoto mgonjwa.

Gavana huyo kupitia ukurasa wake wa Twitter alisifu kazi ya muuguzi huyo aliyetambuliwa kama Elizabeth Robai Lukelesia kutoka taasisi ya Kenya Medical Training (KMTC) Kitale.

“Nimevutiwa na matukio ya kusisimua ya muuguzi wa watoto, Elizabeth Robai Lukelesia kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Kiafya ya Kenya (KMTC) Kitale akimtumbuiza mtoto anayepona. Kazi nzuri Elizabeth, kujitolea katika utoaji wa huduma ndiyo kanuni yetu inayoongoza,” gavana Natembeya alisema.

Lukelesia alichangamsha mioyo ya Wakenya wengi mtandaoni ambao walithamini jitihada zake za kuweka tabasamu kwenye uso wa mtoto huyo ambaye alikuwa amelazwa hospitalini.

Hii haikuwa video ya kwanza ya Lukelesia kuweka tabasamu kwenye nyuso za watu, ukurasa wake wa TikTok umejaa densi zinazofanana na za watu tofauti wakiwemo walinzi, waendesha bodaboda na zaidi.

Baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii walipendekeza muuguzi huyo apewe kazi baada ya kumaliza masomo yake huku wengine pia wakisema atatuzwa na gavana.