Gavana Natembeya aahidi kumtuza muuguzi aliyewatumbuiza watoto wagonjwa

George Natembeya aliahidi kumlipia Elizabeth Robai karo kwa kuwa na bidii katika kazi yake

Muhtasari

• Gavana Natembeya alikuwa amevutiwa na video ya Elizabeth akiwachezea watoto wimbo maarufu wa kuwatuliza watoto wa 'Baby Shark' .

• Video ya Elizabeth akiwachezea watoto ilisambaa na kuibua hisia tofauti.

George Natembeya na Elizabeth

Gavana wa kaunti ya Trans Nzoia George Natembeya, ameahidi kumtuza binti ambaye aligeuka gumzo mtandaoni baada ya klipu yake akiwachezea watoto kusambaa.

Binti huyo ambaye ni mwanfunzi wa Kenya Medial Training College( KMTC) alikuwa anawachezea watoto katika wodi ya hospitali ya Kitale.

Natembeya alikuwa amefurahishwa na jambo la Elizabeth Robai kwa tendo lake la wema la kuwachezea watoto hospitalini.

Alimwalika Elizabeth Robai katika ofisi yake ili kumpongeza kwa kazi yake kisha kumpa hakikisho la kumtuza.

"Jioni hii nilimwalika muuguzi wa watoto Elizabeth Robai Lukelesia, mwanafunzi katika Chuo cha mafunzo ya matibabu (KMTC) ambaye alivuma baada ya video yake kusambaa akimtumbuiza mtoto katika hospitali ya Kitale level IV," Natembeya aliandika.

Katika ukurasa wake wa Twitter, Natembeya alizidi kufafanua jinsi atakavyomtuza mrembo huyo.

"Nimeahidi kulipia masomo yake kwa wakati mdogo uliobaki ili kumaliza masomo yake. Nitahakikisha kuwa ataajiriwa kama mwanafunzi ili kupata mafunzo kisha kutambulika na kuweza kuhudumu kama mwuguzi wa watoto. Hongera Elizabeth Robai, bidii na kujitolea kwako imezaa matunda," Gavana huyo alisema.

Kabla ya kukutana na binti huyo, Gavana Natembeya alikuwa ametangaza jinsi alivyokuwa amevutiwa na jambo hilo.

"Nimevutiwa na matukio ya kusisimua ya muuguzi wa watoto, Elizabeth Robai Lukelesia akimtumbuiza mtoto anayepona.Kazi nzuri Elizabeth, uwajibikaji katika utoaji wa huduma ndiyo kauli mbiu yetu kuu," George Natembeya aliandika.