Mutahi Ngunyi:Orengo anapaswa kuwania urais 2027

Orengo ni wakili mkuu na mwanasiasa ambaye amehudumia Wakenya katika nyadhifa nyingi tofauti.

Muhtasari
  • Orengo alichaguliwa tena kuwa mbunge mnamo Desemba 1992 kwa tikiti ya Ford-Kenya na alichaguliwa tena Desemba 1997

Mchanganuzi wa kisiasa Mutahi Ngunyi amesema kuwa Gavana wa Siaya James Orengo anafaa kuwania kiti cha urais 2027.

Katika taarifa ya Jumatatu, mchanganuzi huyo wa masuala ya kisiasa alisema Orengo anaweza kuweka historia kama vile Rais William Ruto.

"Nadhani Jimmy Orengo anafaa kuwania urais 2027, Nampenda huyu jamaa. Ruto ametuonyesha kuwa haiwezekani sio lolote," alisema.

Orengo ni wakili mkuu na mwanasiasa ambaye amehudumia Wakenya katika nyadhifa nyingi tofauti.

Alichaguliwa kuwa mbunge wa eneo bunge la Ugenya katika uchaguzi mdogo wa mwaka wa 1980, na kumfanya kuwa mbunge mdogo zaidi akiwa na umri wa miaka 29.

Orengo alichaguliwa tena kuwa mbunge mnamo Desemba 1992 kwa tikiti ya Ford-Kenya na alichaguliwa tena Desemba 1997.

Aliwania urais mwaka 2002 kwa tiketi ya Chama cha Social Democratic Party lakini akashika nafasi ya nne.

Mnamo 2013, aliapishwa kama seneta wa Siaya na akachaguliwa tena 2017.