Wape wachungaji kazi, maombi yao yalikufanya rais - Ichung'wah amsihi Ruto

Askofu William Kotut alikuwa awali amemuomba rais Ruto kumpa kazi katika moja ya idara za serikali.

Muhtasari

• Walituunga mkono kwa maombi na umekiri hapo awali kwamba usingekuwa rais lau si kwa maombi, na ni kweli - Ichung'wah alitetea kauli yake.

Mbunge wa Kikuyu akimtaka rais Ruto kuwapa wahubiri kazi za serikali
Mbunge wa Kikuyu akimtaka rais Ruto kuwapa wahubiri kazi za serikali
Image: facebook

Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wah amemtaka Rais William Ruto kuzingatia kuwapa wahubiri nafasi za kazi ili wamuunge mkono katika safari yake ya urais.

Akizungumza wakati wa maombi ya shukrani ya madhehebu mbalimbali huko Kabarnet, Kaunti ya Baringo, Jumapili, mbunge huyo alisema makasisi walikuwa na mchango mkubwa katika ushindi wa Ruto katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti.

Wakati wa mahubiri yake katika uwanja wa maonyesho wa Kabarnet ASK, Askofu William Kotut wa Kanisa la Africa Inland Church alimtaka rais kuzingatia ustawi wa wachungaji.

“Alichokuwa anaomba Askofu Kotut, nimemsikia akiomba kazi na nataka umtafutie yeye na wachungaji wengine kazi. Walituunga mkono kwa maombi na umekiri hapo awali kwamba usingekuwa rais lau si kwa maombi, na ni kweli. Maombi yao yalikufanya uwe rais,” Ichung’wah alisema.

Mbunge huyo wa Kikuyu pia alimtaka Ruto kuchukua hatua haraka kuhusu ukosefu wa ajira na ulevi miongoni mwa vijana.

"Pia amebainisha matatizo makubwa kama vile ukosefu wa ajira kwa vijana, matumizi mabaya ya dawa za kulevya na pombe, pamoja na rushwa," alisema.

Huku akirejelea kisa cha kibiblia cha usaliti wa Joseph na kaka zake, Ichung’wah alidai kuwa Ruto alishinda kinyang’anyiro cha urais wa Agosti 9 licha ya “kusalitiwa” na kaka ambaye hakutajwa jina.

Alitaja ushindi wa Ruto kama zawadi maalum kutoka kwa Mungu kuokoa Wakenya kutoka kwa changamoto za nchi.

Awali wakati wa mahubiri, askofu huyo mkongwe aliyeheshimiwa na marais wa awali kama Daniel Moi na Mwai Kibaki alimtaka rais Ruto pia anapopatiana kazi katika idara za serikali asimsahau.

“Tunakuomba uendelee kuangalia Baringo wakati una mambo mengine, na kama nilivyosema siku nyingine, niangalie mimi pia!” askofu William Kotut alisema.