Migori: Mwanaume akamatwa akijifanya mwanamke, ajiita Sheila kumbe ni Jared

Mwanaume huyo alikuwa amevalia rinda la njano na alijitambua kwa polisi kama Sheila, baada ya usaili wa muda alitoa kitambulisho kilichoonesha jina la kiume.

Muhtasari

• Wananchi walimiminika katika kituo cha polisi kumtambua mtu huyo waliyeamini ni mshukiwa wa maujai ya wakaazi siku za hivi karibuni.

Mwanaume aliyejifanya mwanamke
Mwanaume aliyejifanya mwanamke
Image: Hisani

Maafisa wa upelelezi katika Kaunti ya Migori mnamo Jumatatu walimkamata mshukiwa wa kiume akijifanya mwanamke.

Mwanaume huyo aliyetambulika kwa jina Jared Opiyo Nyatumba, 21, alikamatwa akiwa amevalia nguo ya manjano na alikuwa amechana nywele zake vizuri.

Kulingana na taarifa ya polisi, Opiyo alikuwa akipita karibu na kituo hicho wakati afisa mmoja aligundua kuwa ‘anaonekana kuwa mwanamume’.

"Mtu huyo aliitwa na, baada ya kuhojiwa, alijitambulisha kama Sheila Bichange, mwanamke. Alipofanyiwa uchunguzi wa harakaharaka, alikubali na kutoa Kitambulisho cha Kitaifa chenye picha inayolingana na mwonekano wake na ilionyesha ni Jared Opiyo Nyatumba, mvulana wa Kiluo mwenye umri wa miaka 21 kutoka Kaunti ya Homa Bay,” Nation walinukuu ripoti ya Polisi  kwa sehemu.

Kufuatia kukamatwa kwake, polisi wanasema kuwa wakaazi wa Awendo walimiminika kituoni hapo ili kubaini mtu wanayemshuku kuwa ndiye aliyehusika na mauaji ya hivi majuzi katika eneo hilo na ambaye inasemekana wakati mwingine alijigeuza kuwa mwanamke.

"Mshukiwa alionyeshwa kupitia dirisha la ofisi ya ripoti, lakini walisisitiza kwamba anapaswa kukabidhiwa kwao kwa kuuawa," ripoti ya Polisi ilisoma.

Umati huo ulipoishiwa nguvu, iliwalazimu kutawanywa kwa nguvu na askari wa kupambana na ghasia waliotumia vitoa machozi.

Hii si mara ya kwanza wanaume wametumbuliwa nchini wakiigiza kama wanawake. Wiki chache zilizopita, mwanaume mmoja alifichuliwa na aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko kwa kusemekana kutumia muonekano wake wa kike akijifanya mwanamke. Mwanaume huyo alikuwa anawarubuni na kuwalaghai wanaume pesa zao wakifikiria ni mwanamke mrembo.