Mwanamke kifo chake kilichapishwa kwenye gazeti ajitokeza kuthibitisha yu hai

Tangazo la kifo chake lilichapishwa Novemba 14 na shirika la NMG lilisema alifika katika afisi zake na kupinga madai hayo akisema yu hai.

Muhtasari

• Tangazo hilo la kifo, ambalo limebatilishwa, lilichapishwa kwa mara ya kwanza katika toleo la Novemba 14 la gazeti hilo.

Image: Twitter//Jackson Otukho

Shirika la habari la Natuion nchini Kenya limeomba radhi baada ya kuchapisha taarifa za tanzia za mwanamke mmoja ambaye baadae alijitokeza kusema kuwa hajafa bali yuko hai.

Kupitia toleo lake la magazeti ya Jumatatu, Novemba 14, tangazo la kifo lilitolewa likibainisha kuwa mwathiriwa alifariki Novemba 8, baada ya kudaiwa kuugua saratani.

NMG kupitia barua ya kuomba msamaha ambayo walichapisha kwenye Twitter yao ilibaini kuwa mtu huyo 'aliyekufa' alienda katika ofisi zake baada ya kuchapishwa na kuthibitisha kuwa bado yuko hai.

Tangazo hilo la kifo, ambalo limebatilishwa, lilichapishwa kwa mara ya kwanza katika toleo la Novemba 14 la gazeti hilo, na kufikia Alhamisi asubuhi uongozi wa NMG uliomba radhi na kusema tangazo hilo lilichapishwa baada ya kukabidhiwa maelezo ya uongo.

“Kampuni inasikitishwa na uchapishaji huo na inapenda kuwaomba radhi Rosemary Wakosasa, wanafamilia yake ambao hawakuhusika katika uchapishaji wa notisi hiyo na wananchi kwa usumbufu, mshtuko na aibu waliyoipata kutokana na taarifa za uongo za kifo hicho, tukio la bahati mbaya," kampuni hiyo ilisema katika kuomba msamaha iliyochapishwa kwenye gazeti mnamo Alhamisi, Novemba 17 na pia kwenye Twitter.

Kulingana na NMG, uchapishaji huo ulitolewa baada ya taarifa za uongo kutolewa na mtoto wa mwathiriwa. Kufuatia uchapishaji huo wenye makosa, NMG iliahidi kushughulikia suala hilo kwa mawasiliano na mamlaka husika.

“Tumemchukulia hatua za haraka aliyehusika na uwekaji wa tangazo hilo ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa mamlaka kwa hatua zaidi,” ilisisitiza NMG.

Hasa, Wekosasa alikuwa mfanyakazi wa serikali na alistaafu mnamo 2020 kabla ya kuhamia Nairobi kuwa na mamake.

Kulingana na tangazo hilo la uongo la kifo, Wekosasa alizaliwa mwaka wa 1955 na kukulia Nairobi kabla ya kuhamia Mombasa. Ana mtoto mmoja tu, wa kiume. Wekosasa pia ni binti mzaliwa wa kwanza na mjane.

Mnamo Mei 2019, Mahakama Kuu ya Nairobi iliamuru Nation Media Group kumlipa bilionea Jimmy Wanjigi na mkewe Irene Nzisa jumla ya Ksh8 milioni kutokana na tangazo ghushi la maiti iliyodai kuwa amefariki.