Serikali yadhibitisha Gachagua ndiye mmiliki halali wa ardhi ya Ksh 1.5bn yenye mzozo

Ardhi hiyo iliyopo eneo la Embakasi Nairobi imekuwa ikizozaniwa na kampuni ya Gachagua dhidi ya afisa mstaafu Michael Ohas.

Muhtasari

• Walisema kuwa hati ya umiliki ya DP ilikuwa ya kweli na ni sehemu ya rekodi za Masjala ya Ardhi tangu 2012, ilipotolewa.

DP Gachagua adhibitishwa kuwa mmiliki halali wa ardhi yenye mzozo Nairobi
DP Gachagua adhibitishwa kuwa mmiliki halali wa ardhi yenye mzozo Nairobi
Image: Facebook

Wizara ya Ardhi nchini hatimaye imevunja ukimya kuhusu mzozo wa ardhi ya thamani ya shilingi bilioni 1.5 unaomhusisha naibu rais Rigathi Gachagua.

Kulingana na taarifa za ndani, Afisa mkuu katika Wizara ya Ardhi alisema Jumatano kuwa kipande cha ardhi cha Ksh bilioni 1.5 katika Kaunti ya Nairobi katikati mwa mzozo ni mali ya Wamunyoro Investments Limited, kampuni inayohusishwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Msajili Mkuu Msaidizi wa Ardhi Nyandoro David Nyambaso alisema hatimiliki iliyokuwa na kampuni ya Columbus Thousand Limited ilitolewa kinyume cha utaratibu kwa vile ile ya Wamunyoro Investment Limited ilikuwa tayari ipo na haijafutwa kisheria.

"Katika hali hii, hati miliki iliyokuwa na kampuni ya Columbus Thousand Limited inafaa kughairi isipokuwa mahakama itamke vinginevyo," alisema Bw. Nyambaso.

Walisema kuwa hati ya umiliki ya DP ilikuwa ya kweli na ni sehemu ya rekodi za Masjala ya Ardhi tangu 2012, ilipotolewa.

Naibu rais alihamia kortini dhidi ya afisa katika Wizara ya Ardhi kuhusu umiliki wa kipande cha ardhi huko Embakasi. Ardhi hiyo yenye thamani ya KSh bilioni 1.5 kwa muda mrefu imekuwa katikati ya mzozo kati ya DP na Micheal Ohas, mtumishi wa umma aliyestaafu.

Katika kesi hiyo, DP Gachagua kupitia kwa wakili wake Philip Nyachoti, alikuwa anadai kuwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Mipango ya Kimwili John Michael Ohas alihujumu rekodi katika afisi ya ardhi kwa nia ya kumwibia mali hiyo.

Mali hiyo, anasema, inatozwa kwa Benki ya Equity kama dhamana ya vifaa mbalimbali vya kifedha alizopewa vya jumla ya Ksh.200 milioni.

Hapo awali, Naibu Rais alimpongeza Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kwa hatua ya kufuta kesi ya ufisadi ya KSh bilioni 7.4 dhidi yake. Mnamo Alhamisi, Novemba 10, mahakama ya kukabiliana na ufisadi ilimpa DPP haki ya kufuta kesi ya ufisadi dhidi ya Gachagua.