(+video) Museveni afichua kutetemeka alipoketi karibu na majaji Koome, Mwilu

Alikuwa akizungumzia siku aliyoudhuria kuapishwa kwa rais Ruto mnamo Septemba 13 katika uwanja wa Kasarani.

Muhtasari

• Nilikuwa nimewaona kwenye TV kwamba walihusika katika kesi ya kikatiba. Nikasema nitawezaje kukaa karibu na hawa wanawake wenye nguvu. Nilikuwa nikitetemeka." Museveni alifichua.

Rais wa muda mrefu wa Uganda Yoweri Museveni kwa mara ya kwanza amezungumzia kile alichopitia wakati alihudhuria hafla ya kuapishwa kwa rais wa Kenya William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua mnamo Septemba 13 katika uga wa Kasarani Nairobi.

Katika klipu moja ya video ambayo imesambazwa mitandaoni na haijajulikana ni lini na wapi alikuwa akiyazungumza hayo, Museveni alisema kwamba baadhi ya viongozi walimfanya kuketi karibu na jaji mkuu Martha Koome na naibu wake Philomena Mwilu, jambo ambalo lilimpa mchecheto na woga usiomithilika.

Kiongozi huyo wa National Resistance Movement (NRM) alifichua kwamba amekuwa akiwaona kwenye runinga majaji hao yajika na wakati wa kesi ya kupinga uchaguzi wa urais katika Mahakama ya Juu lakini siku hiyo alikutana nao kwa mara ya kwanza. Licha ya kuwa jenerali mstaafu, Museveni alikiri kutetereka mbele yao wakati wa hafla hiyo.

“Hivi majuzi nilialikwa nchini Kenya kuhudhuria kuapishwa kwa mheshimiwa Arap Ruto. Kwa sababu wanadhani mimi ni mzee, mmoja wa wakubwa alinifanya niketi karibu na meza kuu. Na ni nani aliyeketi karibu nami? wenye nguvu sana. Nilikuwa nimewaona kwenye TV kwamba walihusika katika kesi ya kikatiba. Nikasema nitawezaje kukaa karibu na hawa wanawake wenye nguvu. Nilikuwa nikitetemeka." Museveni alifichua huku umati wa watu wakicheka.

Rais huyo wa Uganda katika siku za hivi karibuni amekuwa akinukuliwa kwa matamshi ya ucheshi ambapo juzi alisikika akikiri wazi kuwa yeye katu hawezi kumpa busu mkewe hadharani, kitu alichokiita kama ni kinyume na mila na tamaduni za Kiafrika.