Karua aapa kupambana na 'udikteta' wa Ruto, arejelea wimbo wa Juliani, "Utawala"

Maadamu nina pumzi, nitapaza sauti yangu kila inapobidi - Karua alisema.

Muhtasari

• Ukimya wetu utamfanya dikteta kuwa mbaya zaidi kuliko tulivyowahi kuona. - Karua.

Karua asisitiza msimamo wake kuwa Ruto hakushinda urais
Karua asisitiza msimamo wake kuwa Ruto hakushinda urais
Image: Screengrab//YouTube

Kiongozi wa chama cha Narc Kenya ambaye pia alikuwa mgombea mwenza wa urais wa Raila Odinga, Martha Karua kwa mara nyingine amemmwagia maji baridi rasi William Ruto kichwani kwa kusema kwamba kiongozi huyo wa taifa anapanga udikteta nchini.

Akizungumza katika kongamano la wanaharakati wa Uganda lililofanyika jijini Nairobi katika jumba la Ufungamano, Karua alisema hata hivyo, hayupo tayari kunyamaza akiongalia maovu hayo ya rais Ruto yakitawala.

Karua alisema kwamba muda wote yeye hupata himizo kutoka kwa wimbo wa msanii aliyetunga wimbo wa kiharakati, Juliani.

“Mimi nahisi kuna kushuka kwa viwango vya uhuru kote duniani na Kenya hali hiyo haijasazwa. Ninaona kufanywa kwa dikteta nchini Kenya. Kesi zinazoondolewa. Kesi za utapeli, mauaji, chochote kile, kuondolewa ambapo watuhumiwa ni watu walio madarakani. Unyakuzi wa ardhi, hati za kiapo zikiapishwa zinazosema hakuna unyakuzi,” Karuac alisema.

Aliendelea, "Kuna kitu kinapika nchini Kenya, na huu ni utengenezaji wa udikteta. Ukimya wetu utamfanya dikteta kuwa mbaya zaidi kuliko tulivyowahi kuona. Sitanyamazishwa, nikichochewa na maneno ya wimbo wa Juliani, "Sitasimama maovu yakitawala".

Bi Karua alibainisha, “Maadamu nina pumzi, nitapaza sauti yangu kila inapobidi, na ninainua kwa mshikamano na Uganda hadi tukomeshe aina yoyote ya ukandamizaji, uvunjaji wa sheria na utekaji nyara wa serikali nchini Kenya na Afrika Mashariki.”

Aliongeza, “Inaanza na viongozi kufikiri wanamiliki Serikali. Wananchi wanamiliki serikali. Sote tuseme hakuna nafasi ya udikteta Afrika Mashariki.”