Winnie asema ushindi wake ni kwa waathirika wa ghasia za baada ya uchaguzi 2017

Watu walimshambuliwa kwa kusema kuwa ushindi wake unaenda

Muhtasari

• Winnie alisema ushindi wake huo unaenda moja kwa moja kama kumbukumbu kwa wale wote walioumia katika vurugu za kisiasa 2017.

Mbunge wa EALA, Winnie Odinga
Mbunge wa EALA, Winnie Odinga
Image: Twitter

Bintiye kiongozi mkongwe wa kisiasa nchini Raila Odinga, Winnie Odinga ametoa tamko lake la shukrani baada ya kuwa miongoni mwa wale waliofanikiwa kuingia katika orodha ya mwisho ya wanasiasa watakaoiwakilisha Kenya katika bunge la ukanda wa Afrika Mashariki, EALA.

Mara tu baada ya kuteuliwa, Winnie kupitia ukurasa wake wa Twitter alionesha kufurahi kwake na kuwashukuru wote waliomuaminia licha ya pingamizi kali kutoka baadhi ya viongozi waliopiga kupendekezwa kwake na muungano wa Azimio la Umoja One Kenya kwa kigezo kuwa ni mtoto wa Odinga.

Winnie alisema ushindi wake huo unaenda moja kwa moja kama kumbukumbu kwa wale wote walioumia katika vurugu za kisiasa zilizoshuhudiwa miaka mitano iliyopita Nairobi baada yake na babake Raila kurejea nchini kutoka ughaibuni – wakati ambapo joto la kisiasa lilikuwa limevuma nchini kutokana na muungano wa NASA kipindi hicho ukiongozwa na babake kupinga vikali matokeo ya uchaguzi wa urais.

“Miaka mitano iliyopita hasa leo, tulipoondoka JKIA, watu 49 walipoteza maisha. Bado niko hapa kwa neema ya Mungu. Leo hii, nimechaguliwa kuwa mwanachama wa EALA. Nimenyenyekea. Nashukuru. Niko tayari. Hii ni kwa wale wote tuliowapoteza njiani. Hakuna mimi bila wewe,” aliandika Winnie.

Matamshi yake hayo yalionekana kutowafurahisha baadhi ya watu ambao walimsuta kwa dhana kuwa alipata tikiti kwenda EALA kwa kivuli cha watu waliokufa wakipigania Odinga.

“Kwa hiyo unawakumbuka wale waliopoteza maisha kwa kuwa umeteuliwa kwenda EALA?” mmoja kwa jina Victor Okuna alimuuliza.

“Anamaanisha watu waliouawa 5yrs ago damu yao ilikuwa dhabihu na kwamba kilichokuwa kinampigania, amesafishwa kwa damu ya Wakenya maskini waliouawa wakati huo,” Mcgriffins aliandika pia.